Mar 24, 2021 12:21 UTC
  • Sisitizo la Russia na China juu ya kurejea bila masharti Marekani katika mapatano ya JCPOA

Wang Yi na Sergei Lavrov, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa China na Russia Jumatatu wiki hii tarehe 22 Machi walisiistiza udharura wa kurejea Marekani katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA bila ya masharti yoyote na kuondolewa vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Iran.

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika katika mji wa Guilin huko China, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi mbili hizo wametangaza kuwa pande mbili hizo zinaamini kuwa, Marekani inapasa kurejea mara moja katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA bila ya masharti yoyote; na kisha iondoe vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Iran. Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Russia na China wameiomba Iran ianze tena kutekeleza mapatano hayo na kusisitiza umuhimu na nafasi ya mapatano ya JCPOA katika kuzuia uenezaji wa silaha la nyuklia duniani. 

Sisitizo la viongozi hao wawili wa ngazi ya juu wa Russia na China kwamba kuna ulazima wa Marekani kurejea katika mapatano ya JCPOA bila ya masharti yoyote limetolewa ikiwa ni msimamo wa pamoja wa Moscow na Beijing kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Russia na China zimesisitiza mara kadhaa udharura wa kuyalinda mapatano hayo na umuhimu wake kwa amani na usalama wa kikanda na kimataifa na pia udharura wa kuepo mlingano baina ya haki na majukumu katika uwanja huo. 

Nchi zilizosalia katika JCPOA baada ya Marekani kujitoa 

Kuhusiana na suala hilo, Moscow na Beijing zinaamini, hatua ya Iran ya kusimaisha utekelezaji wa majukumu yake ndani ya mapatano ya JCPOA ni jibu kwa ukiukaji wa mara kwa mara wa pande za Ulaya yaani kundi la 4+1 na vilevile kwa hatua ya Marekani ya kujitoa katika mapatano hayo mwezi Mei mwaka 2018 na pia ni jibu kwa kitendo cha Marekani cha kuiwekea Iran vikwazo vikubwa zaidi wakati wa utawala wa  Trump. Kwa hiyo Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi mbili hizo wanaitaka Marekani irejeea bila ya masharti yoyote katika mapatano hayo; kwani yenyewe ndio iliyosababisha mivutano iliyopo. 

Ilitazamiwa kuwa baada ya kuingia madarakani, Rais Joe Biden wa Marekani angerejea haraka iwezekanavyo katika mapatano ya JCPOA katika fremu ya misimamo yake ya awali kwamba angerekebisha hatua za rais wa zamani wa nchi hiyo, Donald Trump. Pamoja na hayo, licha ya kupita miezi miwili tangu kuundwa serikali ya Biden, lakini hatua na misimamo inayochukuliwa na viongozi wa ngazi ya juu wa serikali hiyo inaonyesha kuwa, Washington ingali inatekeleza siasa zake zilizofeli za eti mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi dhidi ya Iran kwa matarajio kwamba, itaweza kuilazimisha Iran kutekeleza majukumu yake ndani ya JCPOA bila ya Marekani kutekeleza majukumu yake ndani ya makubaliano hayo.    

Rais Joe Biden wa Marekani  

Joseph Cirincione mchambizi wa masuala ya kisiasa wa Marekani anasisitiza kuwa Biden hivi sasa anaendeleza sera zilizofeli za Donald Trump za mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi dhidi ya Iran. Kuna hatari ya kuyapoteza mapatano hayo muhimu ya nyuklia iwapo Biden hatatekebisha njia yake.  

Serikali ya Biden imesema Iran inapasa kuachana na hatua za ulipizaji kisasi kama sharti lake la kurejea kwenye mapatano ya JCPOA;  ambazo zilichukuliwa na Tehran ikiwa ni jibu kwa kitendo cha Marekani cha kujitoa katika mapatano hayo na baada ya Ulaya kushindwa kutekeleza majukumu yake. Kama alivyosema Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Tehran inataka kuondolewa bila ya masharti vikwazo ilivyowekewa au vilivyorejeshwa dhidi yake na Marekani. Tehran aidha inasisitiza kuwa, haing'ang'anii wala haina haraka na Marekani kurejea kwenye mapatano hayo ya nyuklia. Washington haina haki ya kuainisha masharti ili kutekelezwa mapatano hayo kwa kuzingatia namna ilivyoyakiuka mapatano hayo kwa upande mmoja. Matarajio ya Marekani na washirika wake ambao sasa wanashirikiana na kuchukua hatua kwa pamoja  dhidi ya  Iran, ni kuilazimisha Tehran kuachana na hatua zake za kutotekeleza baadhi ya majukumu yake ndani ya JCPOA bila ya kuitimizia takwa lake kuu ambalo ni kuondoa kikamilifu vikwazo vya Marekani. Pamoja na hayo, msimamo wa Tehran uko imara na haubadiliki. 

Muhamma Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran 

Japokuwa Marekani inadhani kuwa Iran itaachana na sera yake kuu kuhusiana na mapatano ya nyuklia ya JCPOA kwa kupewa baadhi ya vishawishi, lakini mchakato wa uchukuaji hatua wa Iran katika mwenendo wa kupunguza uwajibikaji wake ndani ya mapatano ya JCPOA na hatua zingine zaidi baada ya kupasishwa sheria ya stratejia ya kuondoa vikwazo na kulinda haki za wananchi wa Iran unaonyesha kuwa, Tehran haitasalimu amri wala kulegeza kamba hata kidogo katika kudai na kutetea haki zake.

Tags