Mar 29, 2021 11:09 UTC
  • Antonio Guterres
    Antonio Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekosoa ugavi usio wa kiadilifu wa chanjo ya virusi vya corona duniani na kuzitaka nchi tajiri ambazo zinajilimbikizia kiwango kikubwa sana cha chanjo ya corona kutoa baadhi ya chanjo hiyo kwa nchi nyingine za dunia.

Antonio Guterres ambaye alikuwa akizungumza na televisheni ya CBS ya Canada amesema ana wasiwasi mkubwa kutokana na ugavi huo usio wa kiadilifu wa chanjo ya corona duniani. 
Ametoa wito kwa nchi zilizoendelea kugawana na nchi maskini chanjo ziliyonunua ya corona na kusisitiza kuwa, nchi hizo tajiri zimenunua kiwango ambacho ni zaidi ya mahitaji yao. 

Vilevile ameeleza kusikitishwa kwake na vizingiti vinavyotatiza utekelezaji wa mpango wa Umoja wa Mataiga wa kugawa chanjo ya corona kwa nchi maskini maarufu kama COVAX akitaja ukiritimba wa nchi tajiri, sheria kali zinazozuia uuzaji wa chanjo hiyo na uhaba wa fedha za kutosha za kutekeleza mpango huo. 

Mpango wa COVAX umeanzishwa ili kuhakikisha nchi tajiri duniani hazihodhi dozi zote za chanjo ya corona ambazo kwa sasa zinapatikana kwa kiwango maalumu na kutoweza kukidhi mahitaji ya ulimwengu mzima.

Itakumbukwa kuwa, hivi majuzi viongozi wa Umoja wa Ulaya walipiga marufuku uuzaji wa chanjo ya corona inayozalishwa katika nchi za umoja huo kwenye nchi nyingine.  

Ubaguzi huo katika ugavi wa chanjo ya corona unashuhudiwa huku virusi hivyo vikiendelea kuchukua roho za wanadamu katika nchi mbalimbali za dunia.  

Tags