Apr 05, 2021 02:31 UTC
  • Kuendelea sera za ubaguzi wa rangi barani Ulaya na malalamiko ya wananchi

Suala la Ubaguzi wa rangi limegeuka na kuwa tatizo kubwa kabisa kwa raia wa mataifa ya Ulaya.

Kupanuka wigo wa ubaguzi wa rangi katika mataifa mbalimbali ya Ulaya kama Ufaransa na Uingereza hususan katika miezi ya hivi karibuni sambamba na kuenea virusi vya Corona ulimwenguni, kumewafanya akthari ya wananchi barani humo kujitokeza na kufanya maandamano makubwa ya kulalamikia ubaguzi huo.

Kuhusiana na hilo, wananchi wa mji mkuu wa Uingereza London, usiku wa Jumamosi walijitokeza barabarani na kulalamikia ubaguzi wa rangi nchini humo. Wananchi hao walipaza sauti na kupiga nara za kutaka kuchukuliwa hatua za kukabiliana na aina yoyote ile ya ubaguzi.

Maandamano hayo yamefanyika katika hali ambayo, kupasishwa muswada wa kuliongezea mamlaka jeshi la polisi nchini Uingereza kumeibua hasira na ghadhabu za wananchi wa nchi hiyo. Miamala na vitendo vya kibaguzi vya polisi ya Uingereza hususan dhidi ya watu wenye asili ya Afrika na kuenezwa ripoti za miamala ya kikatili dhidi ya watu weusi ni jambo ambalo limewatia wasiwasi mkubwa wananchi wa Uingereza.

Ukandamizaji wa polisi ya Ufaransa

 

Katika fremu hiyo, hivi karibuni wanasheria 700 na wahadhiri mahiri wa vitivo vya sheria katika Vyuo Vikuu vya Uingereza, walitoa taarifa ya pamoja ilioitaja hatua ya kuliongezea mamlaka jeshi la polisi kuwa ni ya kidhalimu.

Vitendo vya ubaguzi wa rangi haviishi nchini Uingereza tu, bali vimeenea na kusambaa katika mataifa mengine barani Ulaya. Vitendo vya kikatili vya akthari ya raia wa mataifa hayo na hata polisi dhidi ya wahajiri, watu wenye asili ya Afrika, jamii za walio wachache, wafuasi wa dini za walio wachache, wanawake na kutopata raia hao haki sawa za huduma kama chanjo ya Corona, elimu na kadhalika ni mambo ambayo yameweka wazi madai matupu ya akthari ya nara za mataifa hayo katika uga wa kuheshimu na kufungamana na haki za binadamu na kuheshimu suala la haki sawa kwa wote.

Lisa Nandy, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa serikali kivuli ya Uingereza kutoka chama cha Leba anasema: Takwimu za kukamatwa kiholela vijana wenye asili ya Afrika nchini Uingereza zinaonyesha kuwa, nchi yetu ingali inakabiliwa na suala la mfumo wa ubaguzi ulioota mizizi.

Uchunguzi wa maoni uliofanywa na Taasisi ya Mumsnet unaonyesha kuwa: Baada ya kupita mwaka mmoja tangu kuzuka virusi vya Corona, wanawake wa Uingereza ndio ambao wamekuwa wakikabiliwa na hatari ya likizo za muda na hatari ya kupoteza ajira ambapo wasiwasi wao kuhusiana na hatima na mustakabali wao umeongezeka mno.

Maandamano ya kupinga ubaguzi

 

Aidha ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, katika hali ambayo kipato cha kati cha wahitimu wenye asili ya Afrika nchini Uingereza ni pauni 50,000, wahitimu wazungu nchini humo kipato chao cha kati ni pauni laki moja.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anaashiria kuongezeka harakati za ubaguzi wa rangi kwa kusema: Vitisho vya harakati na makundi yanayojiona bora na yenye fikra za Kinazi ni kubwa zaidi ya vitisho vya ugaidi wa ndani.

Hayo yanajiri kati hali ambayo, muamala mbaya na wa ukandamizaji wa polisi katika mataifa ya Ulaya dhidi ya waandamanaji umeshadidi mno. Huko Ufaransa na Uingereza, katika miezi ya hivi karibuni jeshi la polisi lilipata rasmi idhini ya kutumia nguvu na mkono wa chuma dhidi ya waandamanaji.

Mwezi Novemba mwaka jana (2020) Ufaransa ilipasisha muswada wa usalama. Muswada huo ulikabiliwa na malalamiko makubwa ndani na nje ya nchi kutokana na kubinya uhuru wa raia na kukiuka mazingira ya mtu binafsi. Kwa mujibu wa muswada huo, polisi ya Ufaransa ina haki ya kutumia aina mbalimbali za kukabiliana na waandamanaji bila ya kupata idhini ya mahakama.

Ukandamizaji wa polisi ya Uingereza dhidi ya waandamanaji wanaopinga muswada wa kuongezewa mamlaka jeshi la polisi

 

Nchini Uingereza nako, hivi sasa kuliko ilivyokuwa huko nyuma polisi ya nchi hiyo ya bara Ulaya wana ruhusa ya kuwakandamiza waandamanaji.

Ukweli wa mambo ni kuwa, katika miezi ya hivi karibuni ambapo mataifa ya Ulaya yamekabiliwa na mgogoro katika sekta ya uchumi na afya na kuongezeka malalamiko ya kijamii, yameamua kutekeleza sera za ubaguzi na utumiaji mabavu dhidi ya wahajiri, raia wenye asili ya Afrika na hata wanawake. Mataifa hayo yamepasisha sheria ya ukandamizaji na kuihalalisha kwa madai ya kulinda polisi na kurejesha usalama.

Inaonekana kuwa, nara za haki sawa kwa wote na kuheshimu haki za binadamu na demokrasia ambazo kwa miaka mingi zimekuwa zikipigiwa debe na viongozi wa bara Ulaya na kuyatuhumu mataifa mengi duniani kwamba, yanakiuka haki za binadamu na demokrasia inaonekana zimetupwa na kusahaulika hasa baada ya kushadidi migogoro ya kijamii katika mataifa hayo. Kuongezeka ubaguzi wa rangi na kusambazwa mikanda ya vidio inayoonyesha unyama na ukandamizaji wa polisi dhidi ya waandamanaji sambamba na kupasishwa sheria mpya zinazowapa mamlaka zaidi polisi ni ushahidi wa wazi wa kuthibitisha madai haya.

Tags