May 06, 2021 10:14 UTC
  • Tahadhari ya Mwanasheria Mkuu wa Marekani Kuhusu ugaidi wa ndani ya nchi hiyo

Mwanasheria mkuu wa Marekani Merrick Garland ametahadharisha kuhusu hatari inayoibuka kwa kasi ya ugaidi wa ndani ya nchi na amelitaka bunge la nchi hiyo, Kongresi, kutenga fedha zaidi kwa ajili ya kufanya utafiti kuhusu kadhia hiyo na pia kwa ajili ya kuwasaka na kuwafikisha kizimbani magaidi wa ndani ya nchi.

Akizungumza mbele ya Baraza la Wawakilishi katika Bunge la Kongresi, Garland amesema: "Sisi tuna wasiwasi kuhusu kuongezeka misimamo mikali inayoandamana na utumiaji mabavu pamoja na ugaidi ndani ya Marekani na hayo ni mambo ambayo yananikosesha usingizi." Ameitaka Kongresi iongeze bajeti ya Wizara ya Sheria kwa dola milioni 85 ili kufanikisha jitihada za kukabiliana na ugaidi wa dani ya nchi.

Ingawa  Garland hakuashiria jina la kundi lolote ambalo linahusika na ugaidi na utumiaji mabavu ndani ya Marekani, lakini taarifa zinaonyesha  kuwa wanachama wa makundi yenye misimamo mikali ya kufurutu ada kama vile "Proud Boys' na "Oath Keepers" walikuwa miongoni mwa watu 400 waliovamia jengo la Bunge la Kongresi mnamo Januari 6 mwaka 2021.

Kundi la "Proud Boys" ni kundi la ufashisti mamboleo la mrengo wa kulia lenye misimamo mikali ambalo linahimiza utumiaji mabavu katika uga wa kisiasa. Genge hilo limetangaza mara kadhaa kuwa linamuunga mkono Donald Turmp, na wafuasi wake walishiriki katika hujuma dhidi ya jengo la Bunge la Kongresi.

Nalo kundi la "Oath Keepers" ni genge la wanamgambo wenye msimamo mikali ya kufuruta ada ambao wanaipinga serikali. Genge hilo linawahimiza wafuasi wake wasitii amri ambazo kwa mtazamo wao zinakiuka katiba ya Marekani.

Bryan Lewin Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti Kuhusu Misimamo Mikali katika Chuo Kikuu cha California anaashiria hujuma dhidi ya Kongresi Januari Sita na kusema: "Makundi ya mrengo wa kulia yenye misimamo mikali yalitumia fursa hiyo kufikisha ujumbe wao."

Wanamgambo wa Proud Boys nchini Marekani

Rais Joe Biden wa Marekani amewataja wafuasi wa Trump waliokuwa wamejizatiti kwa silaha kuwa ni 'magaidi wa ndani ya nchi'. Mtazamo huo wa Biden ni muhimu kwani ni 'kukiri kulikochelewa' kuwa wazungu wenye misimamo mikali ya kibaguzi ni magaidi wa ndani ya nchi.

Inaelekea kuwa nafasi ya makundi ya wazungu wenye misimamo mikali ya kibaguzi na ambao wanajiona kuwa bora kuliko wanadambu wengine wote inazidi kuimarika katika siasa za ndani nchini Marekani na inaelekea kuwa, makundi haya yatapelekea kuibuka vitendo vya utumiaji mabavu na ghasia katika uga wa siasa nchini Marekani.

Indhari ya mwanasheria mkuu wa Marekani imetolewa kwa kuzingatia nukta hiyo. Mizizi ya ugaidi wa ndani ya Marekani inarejea nyuma miongo kadhaa iliyopita na hadi sasa makundi hayo ya ndani ya  kigaidi yamehusika na matukio makubwa ya ugaidi ndani ya Marekani. Aghalabu ya magaidi wa ndani ya nchi huko Marekani ni wanamgambo wahafidhina wazungu ambao ni wabaguzi wa rangi wenye misimamo ya kufurutu ada.

Miongoni mwa wanamgambo hao kuna wafuasi wa serikali za majimbo na huwa wanapinga sera za serikali kuu ya kifiderali.  Aidha miongoni mwao kuna wabaguzi wa rangi, wapinzani wa dini za walio wachache na wapinzani wa wahajiri ambao kimsingi wanataka wazungu wawe ndio pekee wanaotawala Marekani.

Wanamgambo wa kundi la "Oath Keepers" nchini Marekani

Kuchaguliwa Donald Trump kuwa Rais wa Marekani kulikuwa kichocheo kikuu ambacho kilipelekea kupata nguvu makundi hayo ya wazungu wenye misimamo mikali nchini Marekani.

Mitandao ya kijamii pia imekuwa na nafasi kubwa katika kusambaza itikadi potovu za misimamo mikali nchini Marekani. Inasemekana kuwa hivi sasa kuna makundi zaidi ya 1600 ya wazungu wenye misimamo mikali ya kufurutu ada nchini Marekani.

Mbali na makundi kama vile Ku Klux Klan ambalo harakati zake za ubaguzi wa kikatili zinarejea katika karne ya 19 na pia Wanazi mambo leo ambao wamekuwa wakiendesha harakati zao Marekani kwa miongo kadhaa, katika miaka ya hivi karibuni kumeibuka harakati za wazungu wenye misimamo mikali ya kibaguzi kama Proud Boys na Oath Keepers. Makundi kama hayo yamesambaa kwa kasi na yana nafasi muhimu katika matukio ya kisiasa na kijamii Marekani jambo ambalo limepelekea kuibuke wasi wasi mkubwa kuhusu ongezeko la ugaidi wa dani ya nchi nchini humo. 

 

 

Tags