May 14, 2021 10:00 UTC
  • Arsenal yamtetea Elneny kwa kuwaunga mkono Wapalestina, yasema wachezaji wana haki ya kueleza maoni yao

Klabu ya soka ya Arsenal nchini Uingereza imemtetea mchezaji wake Muislamu raia wa Misri, Mohamed Elneny aliyetuma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akiwaunga mkono na kueleza mshikamano wake na watu wa Palestina wanaoendelea kushambuliwa na kuuawa na jeshi la utawala haramu wa Israel.

Siku chache zilizopita Mohamed Elneny alituma ujumbe akisema: Moyo wangu, roho yangu na uungaji mkono wako vipo pamoja na Palestina. 

Msimamo huu wa mwanasoka wa Arsenal, Elneny umemkasirisha sana mjumbe wa Baraza la Mayahudi nchini Uingereza, Tal Ofer mbaye ameiandikia barua idara ya klabu ya Arsenal akiitaka imfungie au kumtoza faini mchezaji huyo aliyetangaza uungaji mkono wake kwa watu wanaoendelea kudhulumiwa wa Palestina. 

Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Arsenal, Vinai Venkatesham, amekataa wito huo akisema kuwa: "wachezaji wa soka wa Arsenal, kama walivyo wafanyakazi wote wa klabu, wanayo haki ya kueleza mitazamo na maoni yao kupitia kurasa zao makhsusi za mitandao ya kijamii."

Itakumbukwa kuwa, wanasoka mashuhuri, wasanii na wacheza wa filamu wa kimataifa wamejitokeza na kulaani jinai na ukatili unaondelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Palestina na Msikiti wa al Aqsa huko Palestina. 

Mtoto wa Kipalestina aliyeuawa na askari wa Israel

Riyad Mahrez, mchezaji wa timu ya soka ya Manchester City ya Uingereza ambaye ni raia wa Algeria, Mmoroco Achraf Hakimi anayesakata kabumbu katika timu ya soka ya Inter Milan ya Italia, Mfaransa Paul Pogba anyechezea klabu ya Manchester United, Mohamed Salah mshambuliaji wa timu ya soka ya Liverpool ya Uingereza, na mchezaji mwenzake raia wa Senegal Sadio Mane, mchezaji wa zamani wa Arsenal Mesut Ozil anayechezea klabu ya Fenerbahce  ya Uturuki na Mfaransa Franck Ribey anayechezea timu ya Fiorentina ya Italia wote wamejitokeza na kulaani vikali uhalifu na mauaji yanayoendelea kufanywa na jeshi la Israel dhidi ya raia wa Palestina. 

Miongoni mwa wasanii na wacheza filamu maarufu waliojitokeza hadharani kulaani ukatili a Israel huko Palestina ni pamoja na Mmarekani Viola Davis aliyewahi kutunukiwa tuzo ya Oscar. Viola ambaye ana wafuasi zaidi ya milioni 7.7 katika mtandao wa Instagram, amesema walimwengu wanapaswa kuzungumzia maafa yanayotokea eneo la Sheikh Jarrah huko Quds inayokaliwa kwa mabavu. 

Tags