May 14, 2021 12:37 UTC
  • Makundi ya kutetea haki za binadamu yapinga uamuzi wa Ufarasa wa kupiga marufuku maandamano dhidi ya Israel

Wanaharakati na makundi ya kutetea haki za binadamu yamepinga uamuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa wa kupiga marufuku maandamano ya kupinga ukatili na mauaji yanayofanywa na Israel dhidi ya watu wa Palestina ambayo yamepangwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii.

Mbunge Elsa Faucillon wa Ufansa amesema kufanya maandamano ni haki inayopaswa kulindwa na serikali ya Paris na wala si kuizuia.
Mbunge huyo amesema, baada ya Ufaransa kunyamazia kimya mashambulizi yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina ni wadhifa wake na wenzake kukemea mashambulizi hayo.

Kwa upande wake Sihame Assbague, mwandishi wa habari aliyeko Paris, amesema "uamuzi wa Darmanin wa kupiga marufuku maandamano yanayowaunga mkono Wapalestina umechukuliwa kwa sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na kutaka kuonesha mshikamano wa kikoloni wa Ufaransa na vikosi vamizi vya Israeli dhidi ya Palestina".

Mkuu wa Kamati ya Haki na Uhuru ya Ufaransa Yasser Louati amewaambia waandishi habari mjini Paris kwamba "watafanya maandamano ya kuwatetea Wapalestina, sawa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na waziri wake wa mambo ya ndani Darmanin wanapenda au la". 

Amesema “Wapalestina wana haki ya kuishi na kujitetea, na ikiwa wanaweza kukabiliana na mabomu na mauaji ya kimbari, sisi tunaweza kustahamili mabomu ya kutoa machozi na kukamatwa kwa ajili yao".

Siku ya Jumatano iliyopita viongozi wa Ufaransa walimkamata rais wa kikundi cha mshikamano na Palestina, Association France-Palestine Solidarite (AFPS), ambaye alikuwa akipanga kuandaa maandamano ya amani mjini Paris.

Kundi hilo limetoa wito wa kufanyika maandamano kwa ajili ya kuwaunga mkono watu wa Palestina wanaoendelea kuuliwa na jeshi la Israel. 
Watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii wamepinga uamuzi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa wa kupiga marufuku maandamano ya kuwatetea Wapalestina na kupinga utawala wa kibaguzi wa Israel. 

Tags