May 17, 2021 08:39 UTC
  • Kikao cha tatu kisicho na tija cha Baraza la Usalama kuhusu Palestina, kuendelea ukwamishaji wa Marekani

Kwa mara nyingine tena, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshindwa hata kulaani jinai za utawala wa Kizayuni kutokana na ukwamishaji wa dola la kibeberu la Marekani.

Jana Jumapili, Baraza la Usalama liliitisha kikao kwa njia ya Intaneti kwa ajili ya kujadili kadhia ya Palestina na jinai zinazoendelea za Israel dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Ghaza na maeneo mengine ya Palestina.

Kikao hicho kiliitishwa kwa ombi la China, Norway na Tunisia ili kujadili vita vinavyoendelea baina ya utawala wa Kizayuni na makundi ya muqawama ya Palestina na hicho kilikuwa ni kikao cha tatu cha baraza hilo katika kipindi cha wiki moja iliyopita.

Katika vikao viwili vilivyopita pia, Marekani ilikwamisha kulaaniwa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina na vilimalizika bila ya kutolewa tamko lolote la pamoja.

Katika vikao vilivyopita, kati ya wanachama 15 wa Baraza la Usalama, wanachama 14 walitoa tamko la pamoja la kutaka kupunguzwa utesi huko Palestina, na Marekani pekee ilipinga.

Rais wa Marekani, Joe Biden

 

Katika taarifa yao kwenye kikao cha tatu cha Baraza la Usalama, nchi za China, Norway na Tunisia zilisema kuwa zinasikitishwa mno na hali mbaya ya wananchi wa Ghaza na kuongezeka mauaji yanayofanywa na Israel dhidi ya raia wa kawaida na zilitaka vita hivyo vikomeshwe mara moja na sheria za kimataifa ziheshimiwe kikamilifu zikiwemo zinazohusiana na haki za binadamu na kulindwa raia wa kawaidha hasa wanawake na watoto wadogo.

Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa China alilaumu misimamo ya Marekani na kusisitiza kuwa, ukwamishaji wa Washington ndio uliopelekea Baraza la Usalama lishindwe kuzungumza kwa sauti moja. 

Amesema, madai ya Marekani ya kutetea haki za binadamu hayana ukweli wowote, yanalaumiwa na jamii ya kimataifa. Katika vita vinavyoendelea Palestina, Waislamu wengi wanauliwa na Israel huku Wamarekani wakifumba macho yao kama vile hawaoni jinai hizo za Wazayuni.

Vile vile ameitaka Marekani ibebe jukumu la ukwamishaji wake wa juhudi za kimataifa za kukomesha jinai za utawala wa Kizayuni huko Palestina.

Msimamo wa wazi kabisa wa Waziri wa Mambo ya Nje wa China kuhusu nafasi hasi na ya kiuadui ya Marekani inayokwamisha juhudi za kimataifa na za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa za kukomesha jinai za Israel dhidi ya Wapalestina na ambazo hazihalalalishiki kivyovyote vile, ni uthibitisho kuwa, serikali ya Joe Biden huko Marekani inajifanya tu ni mtetezi wa haki za binadamu lakini kivitendo ni mvunjaji mkubwa wa haki hizo hasa linapokuja suala la Waislamu na hasa Wapalestina, na hususan wakazi wa Ukanda wa Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Kwa kweli ni kichekeso cha mwaka, madai ya Marekani ya kwamba eti Israel ina haki ya kujilinda na kufanya mashambulio ya kikatili na kinyama dhidi ya watu wasio na ulinzi ambao imewazingira kila upande tangu mwaka 2006 hadi leo hii. 

Jinai za utawala wa Kizayuni hazihalalishiki kivyovyote vile

 

Marekani ina historia ndefu ya kukamishwa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya utawala katili wa Israel. Hadi hivi sasa Marekani imeshapiga kura za veto mara 44 kukingia kifua jinai za utawala wa Kizayuni na mara nyingi Washington inatumia kura hizo za veto mwanzoni kabisa vikao vya Baraza la Usalama kuhusu jinai na ukatili wa Israel.

Hivi sasa pia kama huko nyuma, Marekani imekwamisha Baraza la Usalama kutoa tamko japo la kulaani tu wimbi jipya la mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Palestina. Serikali ya Joe Biden licha ya kudai ni mtetezi wa haki za binadamu, lakini haina tofauti yoyote na serikali zilizopita za Marekani, msimamo wao wote ni mmoja kuhusu kusaidia jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel kwa hali yoyote ile. 

Hata hivyo, msimamo wa serikali ya Biden wa kuunga mkono na kuhami jinai za kutisha za utawala wa Kizayuni wa Israel zinalaaniwa na kulaumiwa hata ndani ya Marekani kwenyewe na kutoka kwa hata wanachama cha chama chake Biden cha Democratic.

Bernie Sanders, seneta wa kujitegemea wa Marekani ametilia mkazo wajibu wa kukomeshwa haraka mashambulizi ya Wazayuni huko Ghaza na amesema, misaada ya kijeshi ya karibu dola bilioni nne za Marekani kwa Israel inatumika kinyume cha sheria. Inatumika katika kuvunja haki za binadamu kwenye eneo hilo.

Tags