May 25, 2021 10:33 UTC
  • Ufaransa yakiri kuhusu utambulisho wa kigaidi wa utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina

Jumapili iliyopita Jean-Yves Le Drian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa aliashiria hujuma ya kinyama iliyofanywa karibuni na utawala haramu wa Israel katika miji kadhaa ya Waarabu katika ardhi unazozikalia kwa mabavu na kutahadharisha dhidi ya ubaguzi wa rangi unaotekelezwa na utawala huo dhidi ya Wapalestina.

Kwa matamshi yake hayo, amekuwa mmoja wa viongozi wa kwanza wa ngazi za juu wa Ulaya kutumia neno la 'apartheid' linalomaanisha ubaguzi wa rangi kuhusu siasa za kibaguzi za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina.

Jean-Yves Le Drian amesema kwamba iwapo utawala wa Israel utadumisha siasa zake kwa msingi wa hali ilivyo sasa, kuna uwezekano mkubwa wa kutokea apartheid katika ardhi za Wapalestina unazozikalia kwa mabavu, kama ambavyo dalili zilizopo zinaoonyesha kuendelea siasa hizo.

Ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi ya juu barani Ulaya kutamka wazi wazi kwamba utawala ghasibu wa Israel unatekeleza siasa za kibaguzi za apartheid dhidi ya Wapalestina. 'Apartheid' ambalo ni neno la Kiholanzi kwa maana ya ubaguzi wa rangi lilitumika sana wakati wa kutekelezwa mfumo wa ubaguzi wa rangi wa makaburu wa Afrika Kusini dhidi ya wazalendo weusi. Katika miaka ya karibuni, ripoti za mashirika na taasisi mbalimbali za kimataifa zimethibitisha wazi kwamba Israel ni utawala iliojengeka katika misingi ya ugaidi na ubaguzi wa rangi.

Jean-Yves Le Drian

Kwa mujibu wa sheria za kimataifa na hasa Mkataba wa Roma uliobuni Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, mfumo wa apartheid ni jinai ya wazi dhidi ya thamani za kibinadamu. Hatua za Israel dhidi ya Wapalestina katika miongo kadhaa iliyopita na hasa katika ardhi unazokalia kwa mabavu tokea mwaka 1967 zimekuwa ni za kuwabagua Waarabu wa Palestina na kuwabana katika maeneo finyu kupitia ujenzi wa uzio wa kibaguzi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Jambo hilo limezishtua taasisi za kimataifa na hasa mashirika ya kutetea haki za binadamu na kuzifanya zizingatie zaidi mateso yanayofanywa na utawala huo dhidi ya Wapalestina wasiokuwa na hatia.

Katika uwanja huo, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch ambalo ni shirika lisilo la kiserikali na lenye makao makuu yake mjini New York Marekani mwishoni mwa mwezi Aprili uliopita lilitoa ripoti yenye kurasa 213 ambapo lilisema kuwa utawala wa Kizayuni ni utawala wa ubaguzi wa rangi na kuitaka mahakama ya ICC iuchukulie hatua za kisheria. Shirika hilo limesema utawala haramu wa Israel umekuwa ukionywa kwa miongo kadhaa kuhusiana na hatari ya kutumbukia kwenye mfumo wa apartheid kutokanba na siasa zake za ukandamizi na ubaguzi dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi na kwamba sasa tayari umepita hatua hiyo na kutumbukia moja kwa moja kwenye mfumo huo wa apartheid.

Kwa mujibu wa Human Rights Watch, watawala wa Isreal wanawakandamiza kinyama Wapalestina wanaoishi katika ardhi zilizoghusubiwa wakati wa kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel mwaka 1948 na vile vile wale wanaoshi katika ardhi zilizotekwa na kukaliwa kwa mabavu na utawala huo mwaka 1967 na kwamba sasa unatekeleza siasa za makusudi za kuwaua kwa umati na kuwabana katika maeneo finyu na yenye idadi kubwa ya watu. Shirika hilo linaendelea kusema kuwa utawala huo unatekeleza siasa kali na za kinyama dhidi ya Wapalestina wanaoishi katika Ukanda wa Gaza na Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan.

Shirika la Human Rights Watch

Marekani ambayo ni muungaji mkono mkuu wa Israel inapinga vikali ripoti za Human Rights Watch kuhusiana na Israel na hasa zile zinazoutaja utawala huo kuwa wa kibaguzi. Alexandria Ocasio-Cortez, mbunge wa Marekani wa chama cha Democrat amekosoa vikali kisingizio kinachotumiwa na viongozi wa Marekani kuwa Israel ina haki ya kujitetea dhidi ya Wapalestina na kusisitiza kuwa madai hayo hayana ukweli wowote bali utawala huo ni mfano wa wazi wa utawala wa kibaguzi. Ocasio-Cortez amekosoa siasa za Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel za kuwalenga kwa makusudi raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza na maeneo mengine unayoyakali kwa mabavu na kusema: Tawala za kibaguzi si tawala za kidemokrasia.

Ala kulli hal, kukiri waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa kuhusu ubaguzi wa rangi wa utawala ghasibu wa Israel kunabainisha wazi kwamba nchi za bara hilo nazo hatimaye zimeamua kukiri kuhusu ukweli huo. Pamoja na hayo swali muhimu linaloulizwa hapa ni kuwa je, ni kwa nini nchi muhimu za Ulaya kama vile Ufaransa, Ujerumani na Uingereza kwa miaka mingi zimekuwa miongoni mwa waungaji mkono wakuuu wanaotoa misaada mikubwa ya kifedha na kijeshi kwa utawala huo na kutetea kwa hali na mali jinai zake dhidi ya Wapalestina kwa kisingizio cha eti kuunga mkono haki yake ya kujilinda?

 

Tags