May 27, 2021 02:20 UTC
  • Waziri wa zamani wa mambo ya ndani wa Uingereza aitaka Conservative itupilie mbali Islamophobia

Waziri wa zamani wa mambo ya ndani wa Uingereza amekishauri chama tawala cha Conservative kujipanga upya kwa kutupilia mbali sera za kupiga vita Uislamu (Islamophobia).

Sajid Javid amefichua kwamba, aliwahi kukataliwa kugombea katika mojawapo ya majimbo ya uchaguzi ya chama hicho cha Conservative kwa sababu tu yeye ni Mwislamu.

Katika makala yake iliyochapishwa na gazeti la The Times, Sajid Javid amekitaka chama hicho kutekeleza mara moja maagizo ya tume huru iliyoundwa kuchunguza tatizo la propaganda chafu dhidi ya Uislamu na ubaguzi na kuwa kigezo chema kwa vyama vingine.

Uchunguzi - ulioongozwa na Swaran Singh, Kamishna wa zamani wa Usawa na Haki za Binadamu - uligundua kuwa chuki na uhasama dhidi ya Waislamu "bado ni tatizo" katika chama cha Conservative.  

Uchunguzi wa Singh uligundua kwamba, Wahafidhina wana "matatizo na Uslamu."

Sajid Javid

Swaran Singh alisema kuwa matamshi ya Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson - ambaye aliwafananisha wanawake wa Kiislamu wenye vazi la hijabu na mabahasha ya barua - yaliwapa watu taswira kwamba, chama cha Conservative hakijali jamii za Waislamu.

Uchunguzi huo uligundua kuwa theluthi mbili ya malalamiko yaliyopokewa na chama cha Conservative yanahusiana na ubaguzi dhidi ya Waislamu na kwamba kuna "hisia za chuki dhidi ya Waislamu" katika ngazi za kikanda.

Tags