Jun 05, 2021 11:51 UTC
  • Viongozi wa Marekani waendelea na madai yao ya kuijenga upya Ghaza

Mwakilishi wa kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ameendeleza madai ya viongozi wa nchi hiyo kuhusu kuujenga upya Ukanda wa Ghaza. Amedai kuwa Washington inafanya juhudi za kukusanya misaada ya kimataifa ya kuujenga upya ukanda huo.

Linda Thomas-Greenfield ametoa madai hayo bila ya hata kugusia jinsi misaada mikubwa ya kijeshi ya Marekani kwa utawala wa Kizayuni inavyotumika katika jinai kubwa mno kwenye historia ya mwanadamu zinazofanywa na Israel dhidi ya watoto, wanawake, vizee na raia wa kawaida wa Palestina.

Matamshi hayo ya Greenfield yametolewa baada ya yale ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken aliyeandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba Washington bado inaheshimu ahadi zake za kufufua uhusiano wake na taifa la Palestina na kuujenga upya Ukanda wa Ghaza.

Malaika wa Mungu, watoto wadogo wasio na hatia, wahanga wakuu wa jinai za Israel na Marekani huko Palestina

 

Matamshi ya viongozi wa ngazi za juu wa Marekani yanatolewa katika hali ambayo Washington ilikwamisha mara nne juhudi za Umoja wa Mataifa za kusimamisha mashambulizi ya Wazayuni huko Ghaza. Madai makubwa yaliyotolewa mara zote na Marekani kuhalalisha uungaji mkono na msaada wake kwa jinai za utawala wa Kizayuni, ni eti Israel ina haki ya kujilinda. Mara zote hizo serikali ya Joe Biden huko Marekani ilitumia kura ya veto kulizuia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lisitoe angalau tamko tu la kulalamikia japo kwa maneno jinai za Israel dhidi ya raia wa kawaida huko Palestina.

Wapalestina 253 wameuawa shahidi katika vita vya siku 12 vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Ukanda wa Ghaza mwezi Mei mwaka huu. Watoto 66, wanawake 39 na wazee 17 ni miongoni mwa raia wa Palestina waliouliwa shahidi katika vita hivyo vya Israel. Wapalestina wengine zaidi ya 1900 walijeruhiwa katika mashambulizi hayo ya kinyama dhidi ya Ghaza. 

Tags