Jun 08, 2021 18:46 UTC
  • Baraza la Waislamu Canada lataka kukomeshwa chuki dhidi ya Uislamu nchini humo

Baraza la Kitaifa la Waislamu wa Canada limetoa wito wa kutokomezwa haraka sera za chuki na kupiga vita Uislamu (Islamophobia) nchini humo baada ya jinai ya kutisha ya dereva mmoja kuwagonga watu watano wa familia moja na kuua wanne miongoni mwao.

Mkuu wa baraza hilo Mustafa Farouk amesema: "Hili ni shambulio la kigaidi katika ardhi ya Canada, na lazima lishughulikiwe hivyo."

Kwa upande wake, afisa wa jamii ya Waislamu wa Canada, wakili Nawaz Taher, amesema, "Lazima tukabiliane na sera za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu, leo na sio kesho, kwa ajili ya watoto wetu, familia zetu na jamii zetu."

Jumapili usiku dereva mmoja mwenye chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini Canada aliua watu wanne wa familia moja na kujeruhi mwingine vibaya, baada ya kuwagonga kwa makusudi na lori lake katika mkoa wa Ontario.

Polisi katika mkoa huo jana Jumatatu ilithibitisha kuwa watu hao waliuawa kutokana na misimamo ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu ya dereva aliyetekeleza unyama huo katika mji wa London, kusini magharibi mwa mkoa wa Ontario.

Kadhalika meya wa mji wa London katika mkoa huo wa Ontario kulikotokea shambulizi hilo la chuki dhidi ya Uislamu, Ed Holder ameutaja ukatili huo kama mauaji ya umati dhidi ya Waislamu.  Amesema, "mzizi wa mauaji hayo ni chuki za dhati zisizo na kifani. Ukubwa wa chuki hiyo unafanya mtu ajiulize, sisi ni nani (watu wa aina gani) kama jiji."

Waliouawa katika shambulizi hilo wametajwa kuwa ni baba wa familia, Salman Afzal, 46; mke wake Madiha, 44; binti yao Yumna, 15; na bibi aliyekuwa na umri wa miaka 74 ambaye jina lake limehifadhiwa. Mtoto mdogo wa kiume wa familia hiyo, Fayez, 9, amejeruhiwa vibaya na amelazwa hospitalini.

Picha ya familia ya Waislamu waliouliwa Canada

Vitendo vya ubaguzi na chuki dhidi ya Waislamu nchini Canada vimeshtadi katika miezi ya hivi karibuni. Septemba mwaka jana, Baraza la Kitaifa la Waislamu nchini Canada lilitoa mwito wa kuchunguzwa mauaji ya Muislamu nje ya msikiti mmoja mjini Toronto, na kusisitiza kuwa mauaji hayo yalichochewa na chuki za kidini.

Tags