Jun 09, 2021 03:09 UTC
  • Mahakama ya UN yashikilia hukumu dhidi ya Mladic, aliyeua Waislamu 8,000 Bosnia

Majaji wa Mahakama ya Jinai za Kivita ya Umoja wa Mataifa wamedumisha hukumu ya kifungo cha maisha jela dhidi ya Jenerali Ratko Mladic, aliyekuwa kamanda wa kijeshi wa Serbia, ambaye mwaka 2017 alipatikana na hatia ya kuagiza na kuongoza mauaji ya maelfu ya Waislamu huko Srebrenica mwaka 1995.

Majaji wa mahakama hiyo ya UN yenye makao yake mjini The Hague nchini Uholanzi walitoa hukumu hiyo jana Jumanne, ambayo si tu imepongezwa na Waislamu wa Bosnia Herzegovina, lakini pia na jamii ya kimataifa.

Hukumu ya jana ilitolewa baada ya jenerali huyo wa zamani wa Jeshi la Bosnia kukata rufaa dhidi ya hukumu ya awali ya kifungo cha maisha jela, iliyotolewa na mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa mnamo Novemba mwaka 2017.

Majaji wa Mahakama ya Jinai za Kivita ya Umoja wa Mataifa hapo jana walitupilia mbali rufaa ya Mladic, uamuzi ambao ni wa mwisho na usioweza kukatiwa rufani tena.

Mladic mwenye umri wa miaka 78, alipatikana na hatia ya mauaji ya kimbari ya Srebrenica ya Julai mwaka 1995 ambapo zaidi ya wanaume Waislamu 8,000 waliuawa katika hujuma ya askari wa Bosnia Serbia.

Makaburi ya maelfu ya Waislamu waliouawa huko Bosnia mwaka 1995

Michelle Bachelet,  Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amepongeza hukumu dhidi ya Mladic na kuitaja kama ushindi mkubwa kwa mkondo wa haki na sheria.

Kadhalika Alice Wairimu Nderitu, mshauri maalumu wa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa UN katika kuzuia mauaji ya kimbari amesema uamuzi huo wa jana dhidi ya Mladic mbali kuwatendea haki wahanga na manusura wa ukatili wa Srebrenica, lakini pia umetuma ujumbe muhimu kwa eneo la Balkan Magharibi, ambako visa vya kukanusha mauaji hayo ya kimbari yameshtadi, mbali na makatili mfano wa Mladic kuonekana mashujaa na kusifiwa.

Tags