Jun 10, 2021 06:50 UTC
  • Biden afuta amri ya Trump ya kuzifungia baadhi ya programu za China

Ikulu ya Marekani, White House imetangaza kuwa, rais wa nchi hiyo, Joe Biden amefuta amri iliyokuwa imetolewa na rais aliyemtangulia, Donald Trump ya kuzifungia baadhi ya programu za simu za mkononi za China.

Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya Marekani wamesema kuwa, jana Jumatano, Joe Biden alifuta amri ya kuzifungia programu za TikTok na WeChat za China iliyokuwa imewekwa na Donald Trump. 

Uamuzi huo umechukuliwa katika hali ambayo Joe Biden hivi sasa yuko ziarani barani Ulaya ambapo imetajwa kwamba suala la kukabiliana na China ndiyo ajenda kuu ya safari yake hiyo.

Hayo yamekuja baada ya Baraza la Senate la Marekani kuendeleza siasa za uadui za nchi hiyo dhidi ya China kwa kupasisha muswada wa kupambana na maendeleo ya kiteknolojia na ustawi ya China.

 

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, muswada huo ulipasishwa Jumanne kwa kura 68 za ndio na 32 za kupinga. Kwa mujibu wa muswada huo, sasa Marekani inaweza kuanzisha rasmi vita vya kupambana na maendeleo na ustawi wa China katika teknolojia tofauti.Hata hivyo suala hilo limezusha mivutano mikubwa ndani ya Baraza la Wawakilishi la Marekani.

Muswada huo unairuhusu serikali ya Marekani kutenga dola bilioni 190 za kuimarisha utafiti na teknolojia ndani ya nchi hiyo. Pia unaruhusu kutengwa dola bilioni 54 kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa bidhaa za ndani na kufanya utafiti katika vyombo vya mawasiliano na utangazaji.

Muswada huo inabidi upasishwe kwanza na Baraza la Wawakilishi na baada ya kupasishwa ndipo upelekwe mbele ya ofisi ya rais wa nchi hiyo Joe Biden autie saini na kuufanya sheria.

Tarehe 3 mwezi huu wa Juni, rais wa Marekani Joe Biden alitoa amri ya wajibu wa kutekelezwa kwa madai ya kujibu vitisho vya mashirika ya zana za kijeshi za China. Katika amri hiyo, mashirika 59 ya China likiwemo la Huawei, shirika la kimataifa la kutengeneza vifaa vya kompyuta pamoja na shirika la sayansi na teknolojia ya anga za mbali ya China, yamewekwa kwenye orodha nyeusi ya Marekani ya kupiga marufuku kuwekeza ndani yake.

Tags