Jun 16, 2021 02:34 UTC
  • Wanahabari wa Afrika wataka Israel iwajibishwe kwa shambulio la Gaza

Waandishi wa habari wa Afrika wameutaka Umoja wa Afrika (AU) ulaani mienendo ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuwashambulia wanahabari wa Palestina, sanjari na kuubebesha dhima kisheria utawala huo kwa jinai zake dhidi ya wanahabari.

Shirikisho la Wanahabari wa Afrika (FAJ) wamelaani suala la kutowajibishwa kisheria utawala wa Tel Aviv, ambao unafurahia kuua na kushambulia waandishi wa habari kila leo.

Katika taarifa, FAJ imezitaka serikali za nchi za Afrika kusimama upande sahihi wa historia, kwa kulaani kwa nguvu zote ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala haramu wa Israel.

Kadhalika Shirikisho la Wanahabari wa Afrika limetangaza uungaji mkono wake kwa waandishi wa habari wa Palestina na miungano yao, na kusisitiza kuwa linaunga mkono mwito wa Shirikisho la Wanahabari Duniani (IFJ), wa kutaka kulindwa na kupewa haki waandishi wa habari wa Kipalestina.

Wanajeshi katili wa Israel wakismshambulia mwanahabari wa Kipalestina

Ikumbukwe kuwa, Mei 15, jengo la ghorofa 11 la al-Jalaa  ambalo lilikuwa na ofisi za mashirika kadhaa ya habari ya kimataifa kama televisheni ya al Jazeera ya Qatar na shirika la habari la Marekani la Associated Press, lilipigwa kwa makombora kadhaa na kubakia majivu, katika shambulio la utawala haramu wa Israel.

Tel Aviv ilidai kuwa, jengo hilo lilikuwa na zana za Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS). Hata hivyo madai hayo yamepingwa vikali na mmiliki wa jengo hilo. 

Tags