Jun 20, 2021 02:21 UTC
  • UN: Watu milioni 41 wako katika hatari ya janga la ukame duniani

Mpango wa Chakula Duniani WFP ambao uko chini ya Umoja wa Mataifa umesema kuwa, tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi hivi sasa idadi ya watu waliokaribia kukumbwa na janga la ukame imeongezeka kutoka milioni 34 hadi milioni 41 katika pembe mbalimbali za dunia.

WFP imeongeza kuwa, njaa na ukame unaotokana na vita na mapigano, kudorora uchumi kutokana na janga la corona na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa ni katika mambo ambayo yanatishia usalama wa mamilioni ya watu duniani.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeongeza kuwa, watu laki tano na 84 elfu katika nchi za Ethiopia, Madagascar, Sudan Kusini na Yemen wamekumbwa na janga la ukame mwaka huu. Hali katika nchi za Nigeria na Burkina Faso pia ni mbaya na ripoti zinasema kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa kutokea janga la ukame katika nchi hizo.

Shirika la WFP ambalo makao yake makuu yako mjini Roma, Italia, vilevile limetahadharisha kwamba, dunia hivi sasa inaelekea upande wa njaa mutlaki, kwani maendeleo yaliyopatikana ama yamekwama au yameanza kurudi nyuma.

Takwimu za WFP zinaonesha kuwa, zaidi ya watu milioni 270 wana uwezekano wa kukumbwa na ukosefu wa usalama wa chakula katika kona mbalimbali za dunia.

Limeongeza kuwa, kunahitajika msaada wa dharura na wa haraka wa dola bilioni 5 kwa ajili ya kuzuia ukame na kudhamini mahitaji ya chakula ya mamilioni ya watu wanaoteseka kwa njaa katika kona na maeneo mbalimbali duniani.

Tags