Jun 20, 2021 03:27 UTC
  • Hamas: Guterres amebariki jinai dhidi ya watoto wa Palestina

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imetangaza kuwa, hatua ya Umoja wa Mataifa ya kutoliweka jina la utawala wa Kizayuni wa Israel katika orodha ya wakiukaji wa haki za watoto ni sawa na kubariki jinai zinazofanywa na utawala huo.

Taarifa iliyotolewa na Hamas imelaani hatua ya Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ya kutoliweka jina la utawala wa Kizayuni wa Israel katika orodha ya kila mwaka ya UN ya wakiukaji wa haki za watoto duniani. Hamas imesema kuwa jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel za kuua, kusweka watu jela, kuteka nyara, kutokuwepo uchunguzi wa wazi kuhusu jinai na uhalifu unaofanywa na utawala huo na jinai ya karibuni ya kuua watoto 66 wasio na hatia katika mashambulizi yake dhidi ya Gaza na mauaji ya watoto yanayofanywa na Israel kila uchao katika barabara na mitaa ya Ukingo wa Magharibi vinatosha kuliweka jina la Israel katika orodha ya wakiukaji wa haki za watoto duniani.

Makumi ya watoto wasio na hatia waliouawa na Israel katika mashambulizi yake ya karibuni huko Gaza

Hamas imesema kuwa kuupendelea utawala wa Kizayuni kunawatakasa na kuwaondoa hatiani viongozi wa utawala huo kuhusu jinai na uhalifu walioutenda. Vilevile imemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kurekebisha kosa hilo kubwa na kuliweka jina la utawala katili wa Israel katika orodha ya fedheha na kutumia nyenzo zote za kimataifa kwa ajili ya kuuadhibu utawala huo na kuwatetea watoto wa Palestina. 

Itakumbukwa kuwa, Ijumaa iliyopita Umoja wa Mataifa uliiweka Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen katika orodha ya makundi yanayokiuka haki za watoto lakini wakati huo huo haikuziweka Saudi Arabia na utawala haramu wa Isrel zinazoua watoto wa Yemen na Palestina katika orodha hiyo.   

Tags