Jun 24, 2021 03:48 UTC
  • UN yatahadharisha juu ya mabavu na ukandamizaji  mkubwa dhidi ya watoto

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusu vitendo vya mabavu na ukandamizaji mkubwa wanaofanyiwa watoto katika mapigano na mizozo ya kijeshi na wakati huu wa janga la corona.

Virginia Gamba Mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayehusika na watoto ameeleza kuwa, vitendo vya mabavu na ukandamizaji mkubwa dhidi ya watoto katika mapigano ya kijeshi vimekuwa vyenye kutia wasiwasi mkubwa katika miaka ya karibuni. Hii ni katika hali ambayo ugonjwa wa Covid-19 pia umezidisha madhara kwa jamii hiyo ya watoto.  

Gamba amesema kuwa, watoto zaidi ya 19,300 walioathiriwa na vita mwaka jana walikuwa wahanga wa vitendo vya udhalilishaji kama kulazimishwa kutumikishwa kama vibarua na kudhalilishwa kijinsia. Bi Gamba ameongeza kuwa, kuwatumikisha kwa nguvu watoto na kuwadhalilisha kijinsia, kuwaua au kuwasababishia ulemavu ni kati ya mifano ya wazi ya ukandamizaji na vitendo vya mabavu dhidi ya watoto vilivyowaathiri aghalabu ya watoto duniani mwaka uliopita wa 2020. 

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa, maambukizi ya corona duniani yamesababisha kushambuliwa shule na kutumiwa kijeshi; jambo ambalo athari zake zimeongezeka mwaka huu kutokana na kufungwa kwa muda shule kufuatia janga la corona lililoathiri nchi mbalimbali duniani.   

Umoja wa Mataifa Jumatatu wiki hii ulitangaza kuwa, mwaka jana wa 2020 zaidi ya watoto 8,500 walitumiwa kama askari vitani katika maeneo mbalimbali duniani; na wengine karibu ya 2,700 waliuawa.

Askari jeshi watoto 

Tags