Jul 01, 2021 07:41 UTC
  • Wanachama wa Baraza la Usalama waitaka Marekani iiondolee Iran vikwazo

Nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zimeitaka Marekani iiondolee Iran vikwazo vyote kwa mujibu wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Nchi hizo zilitoa mwito huo jana Jumatano katika kikao cha kwanza cha ana kwa ana cha baraza hilo tangu kuanza kwa janga la Corona, ambapo pia zimetangaza kuunga mkono mazungumzo yanayoendelea huko Vienna, mji mkuu wa Austria kuhusu utekelezaji kamili wa mapatano hayo ya kimataifa kwa lengo la kuyahuisha.

Hii ni katika hali ambayo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia ameitaka Marekani iiondolee Iran vikwazo vyote kama yanavyosema makubaliano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA ambayo Washington ilikuwa mstari wa mbele kuyafanikisha.

António Guterres ametoa mwito huo katika ripoti yake iliyowasilishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, huku naibu wake, Rosemary DiCarlo akitilia mkazo suala hilo katika kikao cha jana.

Rais Joe Biden anayetekeleza sera za uhasama wa mtangulizi wake, dhidi ya Iran

Vile vile Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika ripoti yake hiyo ametoa mwito wa kurefushwa ruhusa ya biashara ya mafuta kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika mkutano wa jana, DiCarlo alisisitiza kuwa, UN inataka kuona vikwazo hivyo vinafikia tamati kama ilivyoanishwa kwenye JCPOA, kurefushwa kibali cha Iran kuuza mafuta yake nje ya nchi, sanjari na kufanyika shughuli za nyuklia za Tehran kwa mujibu wa makubaliano hayo.

Tags