Ufaransa yakataa kutoa ramani za maeneo iliyofanyia majaribio ya mabomu ya nyuklia Algeria
Baada ya takribani miaka 60 tokea Ufaransa ihitimishe ukoloni na ukaliaji mabavu wa Algeria, taathira za jinai zake katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika zingali zinahisika na wakuu wa Paris hawako tayari kufidia hasara ambazo waliwasababishia Waalgeria.
Tayeb Zitouni, Waziri wa Mujahideen nchini Algeria ameashiria uamuzi wa Ufaransa wa kukataa kuwasilisha ramani za maeneo ambayo ilitekeleza ndani yake majaribio ya mabomu ya nyuklia katika jangwa la Algeria na kusema: "Hadi sasa Ufaransa haijachukua hatua zozote za kuyasafisha maeneo ambayo yana mada za nyuklia wala haijachukua hatua zozote za kibinadamu kuwasaidia walioathiriwa vibaya na majaribio yake hayo ya nyuklia."
Kwa mujibu wa nyaraka zilizofichuka, wakuu wa dola la kikoloni la Ufaransa walifanya majaribio ya mabomu ya nyuklia katika jangwa la Algeria kuanzia mwaka 1960 hadi 1966 ambapo majaribio manne yalifanyika juu ya ardhi na 13 mengine chini ya ardhi.
Hivi karibuni pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria alizungumzia kadhia hii na kusema: "Milipuko ya nyuklia iliyotekelezwa na Ufaransa katika jangwa la Algeria katika muongo wa sitini ilikuwa na nguvu mara nne zaidi ya milipuko ya Hiroshima Japan na eneo hilo linaendelea kukumbwa na janga lililotokana na milipuko hiyo."
Lakini baada ya kupita miongo kadhaa, Ufaransa imekataa kuipatia Algeria ramani za kitopografia kwa ajili ya kubaini ni wapi hasa milipuko ilijiri na pia sehemu zilikozikwa taka za nyuklia. Hii ni katika hali ambayo majaribio kama hayo ya mabomu ya nyuklia yaliyofanywa na Ufaransa nchini Algeria yanahesabiwa kuwa jinai dhidi ya binadamu. Majaribio hayo ya mabomu ya nyuklia yaliacha taathira mbaya sana na kuvuruga maisha ya idadi kubwa ya watu wa Algeria.
Katika maeneo ambayo Ufaransa ilifanya majaribio ya nyuklia, wanakijiji walikumbwa na mawimbi ya miale ya nyuklia lakini bado uchunguzi kamili wa kubaini walivyoathirika haujafanyika.
Professor Abdulkarim Al Abudi katika kitabu chake kuhusu 'Jinai za Nyuklia za Ufaransa katika Jangwa la Algeria' ameitaja jinai hiyo kuwa, 'Holocaust ya kinyuklia ya Ufaransa' na 'Jinai ya kikoloni ya Ufaransa.'
Algeria ilikuwa moja kati ya koloni muhimu zaidi za Ufaransa na hivyo utawala wa Paris ulitenda kila aina ya jinai nchini humo ili kuwakandamiza wapigania ukombozi.
Waandishi wa historia na wanasiasa wa Algeria wanasema kuwa katika zama za ukoloni mbali na kuwa idadi kubwa ya Waalgeria walifurushwa makwao na mali zao kuporwa lakini pia Waalgeria wapatao milioni tano waliuawa kwa umati na wanajeshi katili wa Ufaransa. Aidha maeneo kadhaa ya nchi hiyo yanaendelea kuathiriwa na minunurisho ya nyuklia inayotokana na majaribio ya mabomu ya nyuklia yaliyofanywa na Ufaransa.
Bouzid Boufrioua kamanda wa zamani wa Jeshi la Algeria alizungumzia kadhia hii na kusema: "Majaribio ya chini ya ardhi yalipelekea eneo kubwa kuchafuliwa kwa mada za nyuklia na hadi sasa kuna taka nyingi za nyuklia zilizoachwa katika eneo la majaribio. Taka hizo zina minunurisho ambayo ingali inawaathiri wakaazi mbali na kusababisha hasara kubwa za kimazingira."
Ripoti kadhaa za huko nyuma, za 'Jumuiya ya 13 Februari 1960' ambayo inawasaidia waathirika wa milipuko ya atomiki ya Algeria, zinaonyesha kuwa majaribio hayo ya mabomu ya nyuklia ya Ufaransa yalipelekea watu 42,000 kupoteza maisha. Aidha watoto wengi waliozaliwa baada ya majaribio hayo wana matatizo ya kiafya kama vile nakisi ya viungo, saratani, matatizo ya kiakili n.k.
Ni wazi kuwa kilichojiri Algeria ni majaribio ya silaha za nyuklia ambayo yalifanywa na Ufaransa kwa kutojali athari mbaya kwa wanaadamu na mazingira ili tu kufikia malengo yake ya kujiimarisha kijeshi na kisiasa.
Baada ya jinai yao hiyo ya wazi, si tu kuwa wakuu wa Ufaransa hawajachukua hatua yoyote ya kuomba radhi bali hata hawako tayari kukiri kuwa waliwakosea Waalgeria. Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa miezi kadhaa iliyopita alisema nchi yake katu haitaomba radhi kutokana na jinai ilizozotenda wakati ilipoikalia kwa mabavu Algeria katika karne ya 20.
Hivyo pamoja na kuwa watawala wa Ufaransa wamekuwa wakitoa nara za kuhadaa umma za eti kufungamana na haki za binadamu na usawa wa wanadamu lakini hawako tayari kuomba radhi kutokana na jinai zao.
Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria alisema hivi karibuni kuwa, "sisi tunataka Ufaransa iyasafishe maeneo ya majaribio ya nyuklia." Aidha alisema ameitaka Ufaransa iombe msamaha kutokana na jinai zake za zama za ukoloni.
Inaelekea kuwa, kufichuliwa jinai za Ufaransa katika nchi kama vile Algeria na Rwanda ni kashfa kubwa ya kisiasa kwa nchi hiyo ya Ulaya na ni dhihirisho la jinai zake za zama za ukoloni kwingineko duniani. Maovu hayo yaliyotendwa na Ufaransa ni kinyume cha madai yake ya haki za binadamu, uhuru na usawa kwa wote na ni wazi kuwa nchi hiyo ingali inaendeleza sera zake za ukoloni.