Jul 09, 2021 09:50 UTC
  • Hatua mpya ya Russia ya kuachana na utegemezi wa sarafu ya dola

Wizara ya Fedha ya Russia imetangaza kuwa, imeondoa kikamilifu sarafu ya dola kwenye Mfuko wa Hazina ya Taifa wa nchi hiyo uliokuwa na akiba ya takriban dola bilioni 65 na kuzibadilisha fedha hizo katika sarafu nyingine za kigeni.

Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imesema, hatua hiyo imechukuliwa kwa lengo la kuachana na utegemezi wa sarafu hiyo ya Marekani.

Kabla ya hapo, Waziri wa Fedha wa Russia Anton Siluanov alitangaza kuwa nchi hiyo itapunguza hadi kiwango cha asilimia sifuri akiba yake ya dola, ambayo inachangia asilimia 35 ya Mfuko wa Hazina ya Taifa.

Mfuko wa Hazina ya Taifa (Russian National Wealth Fund), ni mfuko ulioanzishwa kwa ajili ya kuhifadhi akiba ya baadhi ya fedha na hazina ya Russia, ambao ndani yake huwekwa mapato ya ziada yanayotokana na mauzo ya mafuta na gesi; na pale inapohitajika, serikali huwa inatenga sehemu ya akiba hiyo kwa ajili ya matumizi. Kwa sasa mfuko huo una akiba ya karibu dola bilioni 185 na milioni 900.

 

Russia imechukua hatua mpya ya kupunguza na hatimaye kuondoa kabisa utegemezi kwa sarafu ya dola ili kukabiliana na mashinikizo ya vikwazo vya Marekani na utumiaji mbaya wa sarafu hiyo unaofanywa na Washington kama wenzo wa kuiwekea mashinikizo Moscow.

Siku zote Marekani imekuwa ikiitumia dola, ambayo ndiyo sarafu kuu ya kigeni inayotumika katika miamala ya kimataifa, kama silaha ya kuziwekea mashinikizo nchi zingine.

Washington imeutumia vibaya mara kadhaa na kwa maslahi yake utegemezi wa makampuni, mabenki na mifumo ya fedha ya kimataifa kwa sarafu ya dola kama wenzo na silaha ya kuzilazimisha nchi zingine zifuate matakwa yake au kuzibana zisifuate siasa na sera zisizoipendeza nchi hiyo. Jambo hili limezikera si nchi pinzani pekee bali hata nchi waitifaki wa Ulaya wa Washington na kupelekea kujitokeza taratibu fikra ya pamoja kimataifa ya kuzuia mwendelezo wa utumiaji kimaslahi wa sarafu ya dola unaofanywa na Marekani kwa ajili ya kuzishinikiza kiuchumi, kibiashara na hata kifedha nchi zingine hasa zilizo wapinzani au washindani wa nchi hiyo.

Alasdair Macleod, mtaalamu wa masuala ya fedha anasema: Marekani inatumia sarafu ya dola kama silaha. Marekani inajua kwamba mfumo wa kimataifa wa fedha bado haujapata sarafu mbadala ya dola na kwa hiyo inalitumia vibaya suala hili kwa maslahi yake.

Baada ya mgogoro wa Ukraine wa mwaka 2014, Russia imekuwa ikiandamwa mtawalia na vikwazo vikali vya Marekani na Umoja wa Ulaya; na badala ya kupungua, vikwazo hivyo vimeshtadi katika kipindi hiki cha utawala wa Joe Biden.

Rais Vladimir Putin wa Russia

 

Mnamo mwezi uliopita wa Juni, Rais Vladimir Putin wa Russia alitanabahisha kuwa kitendo cha Marekani cha kuitumia sarafu ya dola kama silaha katika vita vya kisiasa na kiuchumi kimeshusha hadhi yake ya kuwa sarafu ya akiba ya kimataifa. Putin alibainisha kwamba, kwa mujibu wa makadirio yaliyofanywa kimataifa, mahitaji ya dola, kama sarafu ya kigeni ya akiba, yamepungua katika nchi nyingi zikiwemo hata nchi waitifaki wa Marekani.

Kimsingi ni kwamba, kupunguza utegemezi kwa sarafu ya dola katika miamala ya malipo kimataifa ni moja ya hatua ya kujibu mapigo iliyochukuliwa na Russia kukabiliana na hatua za kihasama za Marekani; na moja ya sababu za kufanikiwa utekelezaji wa mkakati huo ni makubaliano yaliyosainiwa na kutekelezwa kati ya Russia na nchi zingine kuanzia mwaka 2013 hadi 2018.

Katika kipindi hicho, kiwango cha sarafu ya dola katika mabadilishano ya kibiashara ya Russia kilipungua kwa dola bilioni 388; na mkabala wake, kiwango cha yuro kiliongezeka kwa asilimia 21.9 kwa kiwango cha dola bilioni 151.

 

Utumiaji mbaya wa sarafu ya dola unaofanywa na Marekani ili kutoa pigo kwa nchi nyingine, hata kama katika muda mfupi ujao utaweza kuiwezesha Washington kufikia malengo yake, lakini kwa malengo ya muda mrefu, sera hiyo itakuwa na madhara kwa nchi hiyo. Ni kama inavyoshuhudiwa hivi sasa, ambapo mbali na Russia na China, baadhi ya nchi zingine pia zimeamua kufuata muelekeo huo wa kupunguza matumizi ya sarafu ya dola katika mabadilishano ya kiuchumi na kibiashara, jambo ambalo hapana shaka baada ya muda litasababisha madhara makubwa kwa nafasi ya sarafu ya dola kimataifa…/  

 

Tags