Jul 23, 2021 08:22 UTC
  • Emmanuel Macron, mhanga wa ujasusi wa Wazayuni kupitia programu ya Pegasus

Gabriel Attal, Msemaji wa Serikali ya Ufaransa alisema Alhamisi kuwa Rais Emmanuel Macron aliitisha kikao cha Baraza la Ulinzi siku hiyo hiyo kwa ajili ya kuchunguza na kujadili ujasusi uliofanywa dhidi yake kupitia programu ya Kizayuni ya Pegasus.

Inasemekana kuwa mashirika ya ujasusi ya Ufaransa yalikuwa yamemuonya Macron kuhusiana na suala hilo lakini akawa amelipuuza. Katika siku chache zilizopita maudhui ya Pegasus imegeuka na kuwa suala muhimu zaidi la usalama linalohadiliwa hivi sasa katika ngazi za kimataifa.

Uchunguzi uliofanywa na mashirika 17 ya habari yanayofanya kazi chini ya kundi lisilo la kiserikali la Forbidden Stories lenye makao makuu yake mjini Paris na ambalo lilichapisha matokeo ya uchunguzi huo Jumapili iliyopita, unaonyesha kuwa proghramu hiyo iliyotengenezwa kwa kibali cha shirika la utawala haramu wa Israel la NSO, imefanikiwa au kufeli kudukua simu erevu za waandishi, maafisa wa serikali na wanaharakati wa haki za binadamu wapatao 37 na kwa ujumla imeweza kutumika kulenga simu zisizopungua elfu 50 katika maeneo tofauti duniani.

Wanasiasa mashuhuri kimataifa akiwemo Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Charles Michel, Rais wa sasa wa Baraza la Ulaya ni miongoni mwa wahanga wa programu hiyo ya ujasusi.

Emmanuel Macron mmoja wa wahanga wa programu ya kijasusi ya Wazayuni, Pegasus

Shirika la Kizayuni la NSO limedai kuwa programu hiyo imetengenezwa eti kwa ajili ya kupambana na ugaidi, madai ambayo hayana msingi wowote.

Jake Moore, mtaalamu wa masuala ya usalama anasema: Wahanga wa programu hii ni pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu, waandishi, wanasiasa na baadhi ya matajiri mashuhuri duniani. Kwa msingi huo ni watu mahsusi ndio wanalengwa na programu hiyo.

Vile vile programu ya kijasusi ya Pegasus imeuziwa baadhi ya nchi kama vile Saudia na Imarati na pia imetumika kudukua habari na maelezo ya simu za watu mashuhuri ulimwenguni. Baadhi ya shakhsia muhimu wa kidini, kisiasa na kijeshi wa Iraq pia wamelengwa na programu hiyo ya kijasusi ya Wazayuni.

Kufichuliwa ujasusi unaofanywa kupitia programu ya Pegasus kunathibitisha wazi kwamba utawala haramu wa Israel kwa kisingizio cha kudhamini maslahi yake ya kisiasa, kiusalama na kibiashara katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu, haujali hata kidogo kiziuzia programu hiyo ya kijasusi tawala kandamizi za eneo zikiongozwa na Saudia bali huwa hausiti kufanya ujasusi dhidi ya washirika wake wa Magharibi kama Ufaransa na Umoja wa Ulaya.

Kwa maneno mengine ni kwamba jambo lenye umuhimu kwa utawala ghasibu wa Israel ni kudhamini tu maslahi yake na ili kufikia lengo hilo uko tayari kufanya lolote kukiwemo kufanya ujasusi na kuhatarisha usalama wa washirika wake wa Magharibi zikiwemo nchi za Umoja wa Ulaya.

Nchi ambazo zimenufaika zaidi na programu ya kijasusi ya Pegasus ni Bahrain, Morocco, Saudi Arabia na  Imarati.

Jumanne iliyopita gazeti la Ufaransa la Le Mond lilifichua kwamba vyombo vya usalama vya Morocco vilidukua simu za Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Edouard Philippe, Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo kupitia programu ya Pegasus. Ni wazi kuwa viongozi wa Tel Aviv wanafahamu vyema uwezo wa kijasusi wa programu ya Pegasus na bila shaka waliruhusu nchi kama vile Saudia, Bahrain, Morocco na Imarati ziuziwe programu hiyo kwa ajili ya kutekeleza hatua zisizo za kisheria na hasa kudukua simu za wanaharakati, waandishi, wanasiasa na maafisa wa ngazi za juu katika nchi tofauti. Na hasa ikitiliwa maanani kuwa afisa mmoja wa Marekani ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema kwamba shirika la NSO huwa linaupa utawala haramu wa Israel habari muhimu na za usalama wa kitaifa zinazohusiana na watu mashuhuri duniani. Suala hilo limeamsha hasira ya nchi za Ulaya.

Serikali ya Narendra Modi wa India pia imekumbwa na kashfa ya Pegasus

Angela Merkel, Kansela wa Ujerumani ameashiria uwezo wa kijasusi wa programu ya Pegasus iliyotengenezwa na utawala wa Kizayuni na kutaka hatua kali za kiusalama na kiudhibiti zichukuliwe ili kuzuia kutumika vibaya programu kama hizo zinazodaiwa kuwa ni za kibiashara kwa ajili ya kufikia malengo ya kijasusi dhidi ya watu na usalama wa kitaifa wa nchi nyingine. Ametaka programu kama hizo zitumike tu baada ya kupata kibali cha vyombo vya mahakama. Suala la kuzingatiwa hapa ni kuwa hivi karibuni kulifichuliwa habari nyingine inayosema kwamba Marekani ambayo ni mshirika mkubwa na wa karibu wa utawala wa kibaguzi wa Israel, ilisikiliza kwa siri simu za Angela Merkel na viongozi wengine wa ngazi za juu wa Ujerumani na Ulaya.

Kwa maelezo hayo, inabainika wazi kuwa Washington na Tel Aviv zina mbinu moja katika kuwafanyia hiana washirika na marafiki wao wa karibu kuhusiana na suala zima la kudukua na kusikiliza kwa siri simu zao za mkononi na wala huwa hazisiti wala kuona haya kuhusiana na suala hilo.

Tags