Aug 01, 2021 09:48 UTC
  • UN: Mzingiro wa Israel dhidi ya watu wa Gaza unakiuka sheria za kimataifa

Ripota Maalumu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa huko Palestina amesema kuwa nzingiro wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza unakiuka sheria za kimataifa.

Michael Lynk amesema kuwa, nchi za Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya pia zimekiuka sheria za kimataifa kwa kuipa Israel silaha zinazotumika kushambulia watu wa Gaza na Syria. 

Lynk amesema kuwa, vita na mashambulizi ya mwezi Mei yaliyofanywa na Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza yamesababisha hasara ya dola nusu bilioni na kwamba eneo hilo la Palestina linapata maji safi masaa 14 tu kwa siku. Ripota huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza udharura wa kukarabatiwa uharibifu ulisababishwa na mabomu ya jeshi la Israel katika Ukanda wa Gaza. 

Kuhusu mashambulizi ya karibuni ya Wazayuni huko Palestina, Michael Lynk amesema Baraza la Usalama, Baraza Kuu na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa zimekuwa zikisisitiza kuwa Israel inaendelea kukika haki za binadamu. Amesema azimio nambari 1998 pia linasisitiza kuwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi inayokaliwa kwa mabavu ya Palestina ni sawa na kukanyaga na kukiuka haki za binadamu.  

Watoto wa Gaza waliouawa katika mashambulizi ya karibuni ya Israel

Amesema vitongoji baina ya 200 hadi 250 vya walowezi wa kizayuni vimejengwa huko Mashariki mwa Quds inayokaliwa kwa mabavu na Ukingo wa Magharibi na kwamba jambo hilo ni kizingiti kikubwa cha kuundwa dola huru la Palestina.

Ripota Maalumu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Palestina amegusia pia programu ya ujasusi ya Israel, Pegasus, na kusema: Makampuni ya Kizayuni yamekuwa yakitumia programu kama hizo kwa miongo kadhaa kwa ajili ya kufanya ujasusi dhidi ya Wapalestina. Amesema programu ya ujasusi inayotumiwa leo dhidi ya Wapalestina itatumiwa kesho dhidi ya mataifa mengine ya dunia.   

Tags