Aug 03, 2021 07:50 UTC
  • Tuhuma za Blinken dhidi ya Iran kuhusu shambulio la meli ya utawala wa Israel

Antony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kwa mara nyingine amekariri tuhuma zisizothibitishwa za nchi hiyo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kudai kuwa viongozi wa Washington wanaamini kuwa Iran imehusika katika shambulio dhidi ya meli ya mafuta ya utawala haramu wa Israel.

Waziri huyo amedai kuwa katika miezi ya karibuni Iran imehusika katika matukio kadhaa ya uharibifu yakiwemo ya kushambuliwa meli za mafuta. Antony Blinken amedai katika sehemu nyingine kwamba hatua ya Iran ya kushambulia meli ya Mercer Street katika Bahari ya Oman itakabiliwa na jibu la nchi kadhaa.

Akizungumza katika kikao cha kila siku na waandishi habari hapo jana Jumatatu, Jen Psaki, Msemaji wa White House pia alisema kuhusu shambulo hilo kwamba Israel ni serikali inayojitawala na ambayo ina uhuru wa kuchukua uamuazi unaofaa kuhusu shambulio hilo.

Meli ya Mercer Street iliyoshambuliwa karibuni

Akijibu tuhuma hizo leo Jumanne kupitia ukurasa wake wa Twitter, Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amepinga tuhuma zinazotolewa na utawala wa Kizayuni na viongozi wa nchi kadhaa za Magharibi kuhusu suala hilo na kusema: Iran ikiwa ni nchi muhimu inayolinda amani na usalama wa Ghuba ya Uajemi inapinga na kulaani vikali taarifa za kichochezi ambazo zinatolewa dhidi yake kwa utaratibu maalumu na Uingereza na Marekani.

Amesema nchi hizo hizo za Magharibi ambazo zimekuwa zikinyamazia kimya mashambulio mengi yanayofanywa dhidi ya meli za kibiashara na mafuta za Iran sasa zinatoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya taifa la Iran. Ametahadharisha kwamba chokochoko zozote zitakazofanywa dhidi ya maslahi ya Iran zitakabiliwa na jibu kali na la haraka.

Ikifuata mfano huo huo wa Uingereza na Marekani, Canada nayo imetoa tuhuma kama hizo zisizo na msingi dhidi ya Iran katika ukurasa wake rasmi wa Twitter bila kuwasilisha nyaraka zozote za kuaminika katika uwanja huo.