Mar 02, 2021 02:41 UTC
  • Jumanne, Machi Pili, 2021

Leo ni Jumanne tarehe 18 Rajab 1442 Hijria sawa na tarehe Pili Machi mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1432 iliyopita alifariki dunia mtoto mdogo wa Mtume wetu Muhammad (saw), Ibrahim akiwa na umri wa miezi 18 tu. Ibrahim ambaye alifariki dunia kutokana na maradhi alikuwa mtoto wa kiume pekee wa Mtume ambaye hakuzaliwa na Bibi Khadija (as). Mama yake alikuwa Maria al Qibtiyya ambaye alitumwa na mfalme wa Misri ya wakati huo kuwa hadimu na mtumishi wa Mtume na aliolewa na mtukufu huyo baada ya kusilimu. Kifo cha Ibrahim kilimhuzunisha sana Mtume (saw) kwa sababu mtukufu huyo alikuwa akimpenda sana mtoto huyo. 

Kaburi ya Ibrahim, mtoto wa Mtume Muhammad (saw) katika makaburi ya Baqi'. Madina

Tarehe 18 Rajab miaka 1016 iliyopita alifariki dunia Ibn Samh huko katika mji wa mjini Andalucia. Msomi huyo wa Kiislamu alikuwa mtaalamu wa hesabu, nyota na tabibu. Alizaliwa katika mji wa Cordoba, Andalucia mnamo mwaka 370 Hijiria. Msomi huyu wa Kiislamu alifanya utalii na utafiti mwingi katika elimu za hesabu na nyota, sambamba na kuwalea wanafunzi wa zama zake. Kuna vitabu kadhaa vilivyoandikwa na Ibn Samh kwa lugha ya Kiarabu na miongoni mwavyo ni pamoja na kitabu kiitwacho "Al Madkhalu Ila al Handasah", "Al Muamalat" na "Kitabuz Zayj."

Siku kama ya leo miaka 125 iliyopita sawa na tarehe Pili Machi mwaka 1896 mwanafikizia wa Kifaransa Henri Becquerel alivumbua nururishi au Radioactivity baada ya kufanya utafiti katika mada za urani na vitu vinginevyo. Becquerel alikuwa akichunguza urani ndipo alipogundua nururishi. Utafiti wa mwanafikizia huyo wa Kifaransa ulimfanya atunukiwe tuzo ya Nobel mwaka 1903 na miaka mitano baadae aliaga dunia.

Henri Becquerel

Miaka 65 iliyopita katika siku kama hii, nchi ya Morocco ilipata uhuru. Morocco iko kaskazini mwa Afrika katika Ukingo wa Bahari ya Mediterrania na Bahari ya Antlantic na inapakana na Algeria na Sahara Magharibi. Morocco ilikombolewa na Waislamu mwishoni mwa karne ya Saba Miladia na silsila kadhaa za kifalme zilitawala nchini humo. Mapambano ya wananchi Waislamu wa Morocco dhidi ya wakoloni wa Uhispania na Ufaransa yalipelekea nchi hiyo kupata uhuru mwaka 1956.

Bendera ya Morocco

Siku kama ya leo miaka 17 iliyopita, mwafaka na tarehe Pili Machi mwaka 2004, mamia ya watu wasio na hatia waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika miripuko kadhaa mikubwa iliyotokea katika shughuli ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein (AS) huko katika miji mitukufu ya Karbala na Kadhimein nchini Iraq. Katika mwaka huo wananchi Waislamu wa Iraq walifanya maadhimisho hayo kwa hamasa kubwa baada ya utawala wa Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa nchi hiyo aliyeng'olewa madarakani, kupiga marufuku kwa miaka kadhaa shughuli zote za aina hiyo. Miripuko hiyo ya kigaidi ya Karbala na Khadhimein ilitokea ikiwa ni muendelezo wa machafuko yaliyoikumba Iraq tangu nchi hiyo ivamiwe kijeshi na kukaliwa kwa mabavu na Marekani na Uingereza mwaka 2003. 

 

Tags