Aug 13, 2023 02:55 UTC
  • WHO yaimarisha hatua za kukabiliana na kipindupindu ambacho kimeua watu 30 nchini Somalia

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema limeongeza hatua za dharura ili kuokoa maisha na kuzuia maambukizi zaidi ya kipindupindu nchini Somalia baada ya watu 30 kufariki dunia kutokana na ugonjwa huo tangu Januari mwaka huu.

WHO imesema Somalia imekuwa na maambukizi ya kipindupindu katika wilaya 28 zilizoathiriwa na ukame tangu 2022 na katika eneo la Banadir tangu ukame wa 2017.

Katika taarifa iliyotolewa Mogadishu, mji mkuu wa Somalia, WHO imesema: "Tangu wiki ya 1 ya mlipuko ya 2023, jumla ya kesi 11,704 zinazoshukiwa ni za kipindupindu, ikiwa ni pamoja na vifo vya watu 30 vinavyohusishwa, viliripotiwa kutoka wilaya 28 za Somalia."

WHO imesema baadhi ya washukiwa wapya 235 ambao hawakuhusishwa na kifo waliripotiwa mwishoni mwa Julai kutoka wilaya 28 zilizoathiriwa na ukame.

"WHO na washirika wa afya wameongeza utekelezaji wa hatua za dharura za kukabiliana na kipindupindu katika wilaya zilizoathiriwa na ukame zinazolenga jimbo la Jubaland ambalo ni kitovu cha sasa cha mlipuko wa ugonjwa huo," ilisema taarifa ya WHO.

Umoja wa Mataifa ulionya mwezi Aprili kwamba mafuriko ya ghafla na mito yanayosababishwa na mvua kubwa nchini Somalia yanaweza kuzidisha milipuko ya magonjwa yanayosababishwa na maji.

Tags