Sep 24, 2023 10:52 UTC
  • Marekani yaogopeshwa na ushawishi wa kijeshi wa China barani Afrika

Kiongozi mmoja wa ngazi za juu wa Marekani amesema kuwa, Washington ina wasiwasi mkubwa kutokana na ushawishi wa kijeshi wa China nchini Djibouti.

Akihojiwa na televisheni ya Aljazeera ya Qatar, Waziri wa Ulinzi wa Marekani amesema, nchi yake ina wasiwasi mkubwa kutokana na China kupeleka wanajeshi wake katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Amesema, tuna wasiwasi mkubwa kutokana na uwepo wa kijeshi wa China nchini Djibouti kwani Marekani ina wanajeshi wake huko.

Amma kuhusu matukio ya Sudan, na bila ya kugusia kabisa kwamba baadhi ya silaha zinazotumika kwenye vita vya majenerali wa kijeshi huko Sudan ni za Washington, waziri huyo wa ulinzi wa Marekani amedai kuwa, anazitaka pande hasimu na waungaji mkono wao waache vita na wakae kwenye meza ya mazungumzo. 

Nchi za Afrika zimegeuzwa kuwa uwanja wa kutunishiana misuli madola hasimu

 

Kuhusu matukio ya nchini Niger, Waziri wa Ulinzi wa Marekani amedai kuwa, matumizi ya nguvu za kijeshi nchini humo ni jambo linalotia wasiwasi. Lakini hakugusia kabisa jinsi nchi za Magharibi ikiwemo Marekani na Ufaransa zilivyoichochea kupindukia Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS kutumia nguvu za kijeshi kumrejesha madarakani Mohammed Bazoum ambaye wananchi wa Niger wanamlaumu kwa kuwa kibaraka mkubwa wa mkoloni kizee, Ufaransa.

Waziri huyo wa wizara muhimu sana ya Marekani ameshindwa pia kuficha woga wake kutokana na mapinduzi ya kijeshi yanayowapindua vibaraka wa nchi za Magharibi barani Afrika na ameiambia televisheni hiyo ya Aljazeera kwamba, hata baada ya kufariki duniani mkuu wa kundi la Wagner, Yevgeny Prigozhin, hadi sasa hatujashuhudia kupungua wapiganaji wa kundi hilo, barani Afrika.