Sep 25, 2023 06:09 UTC
  • Thamani ya Pauni ya Sudan yavunja rekodi ya kuporomoka kutokana na vita

Pauni ya Sudan jana ya Jumapili ilivunja rekodi ya kuporomoka thamani mbele ya fedha za kigeni ikisajili kiwango cha chini kabisa cha kubadilisha pauni 880 kwa kila dola moja ya Marekani.

Mfanyabiashara mmoja wa fedha za kigeni katika mji mkuu Khartoum ameliambia shirika la habari la Xinhua kwamba, jana Jumapili kila dola mja ya Marekani ilinunuliwa kwa pauni 880 na kuuzwa kwa pauni 885 za Sudan kiwango ambacho ni cha chini kabisa cha thamani ya poauni. 

Tarehe 14 Aprili yaani kabla ya kuanza vita baina ya majenerali wa kijeshi nchini Sudan, dola moja ya Marekani ilinunuliwa kwa pauni 607 za Sudan.

Mfanyabiashara huyo amesema kuwa, dalili zote zinaonesha kuwa sarafu ya Sudan itaendelea kuporomoka mbele ya sarafu za kigeni kutokana na athari mbaya za vita na kushindwa serikali kutoa fedha kwa ajili ya kuingiza bidhaa na huduma kutoka nje kutokana na fedha zote kutumiwa katika masuala ya vita na mapigano ya kuwania madaraka baina ya majenerali hao wa kijeshi.

Vita vya kuwania madaraka baina ya majenerali wa kijeshi nchini Sudan vinaendelea kuangamiza nchi kila upande

 

Wataalamu wa masuala ya kiuchumi walionya tangu zamani kuwa vita baina ya Jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vitazorotesha mno uchumi wa Sudan na kuporomosha sarafu ya nchi hiyo. 

Zuhair Al-Bakri, mchambuzi wa masuala ya uchumi ya Sudan anasema: "Kuendelea kuporomoka thamani ya pauni ya Sudan mbele ya fedha za kigeni ni kiashirio cha kuporomoka uchumi wa nchi hiyo.

Mtaalamu mwingine wa masuala ya uchumi wa Sudan, Adil Mahjoub alitabiri  tangu zamani kuwa thamani ya pauni ya Sudan kinaweza kupindukia elfu moja  kwa kila dola moja ndani ya miezi miwili ijayo, isipokuwa kama Benki Kuu itachukua hatua madhubuti.