Sep 25, 2023 06:09 UTC
  • Hatimaye Ufaransa kuondoa wanajeshi na balozi wake nchini Niger baada ya kufukuzwa

Rais wa Ufaransa ametangaza kuwa wanajeshi wa nchi hiyo watarejeshwa nyumbani kutoka Niger baada ya serikali mpya ya Niamey kukata uhusiano wake wa kijeshi na mkoloni huyo kizee wa barani Ulaya.

Kwa mujibu wa televisheni ya Al Jazeera, Emmanuel Macron alisema hayo jana jioni na kudai kuwa wameamua kumuondoa balozi wao nchini Niger na kusitisha uhusiano wao wa kijeshi na nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Matamshi hayo ya rais wa Ufaransa yamekuja kwa kuchelewa sana baada ya balozi wa Ufaransa na wanajeshi wa nchi hiyo kutimuliwa huko Niger. 

Macron anadai kuwa wao ndio walioamua kumrejesha nyumbani balozi na wanajeshi wao kutoka Niger katika hali ambayo muda wote huu Paris ilikuwa inafanya ukaidi wa kuondoka katika nchi hiyo ya Afrika licha ya kufukuzwa, kukatiwa maji, umeme na chakula na licha ya kupigwa marufuku mtu yeyote kushirikiana na ubalozi wa Ufaransa mjini Niamey.

Maandamano makubwa ya wananchi wa Niger ya kuunga mkono kutimuliwa wanajeshi na balozi wa Ufaransa nchini mwao

 

Mataifa ya rais wa Ufaransa yamekuja baada ya kufanyika maandamano makubwa ya mara kadhaa ya wananchi wa Niger ya kutaka wanajeshi wa mkoloni huyo wa Ulaya na balozi wake waondoke kwenye ardhi ya Niger.

Kwa mujibu wa Macron, wanajeshi 1,500 wa Ufaransa wataondoka nchini Niger katika kipindi cha wiki na miezi ijayo na watakuwa wote wameshaondoka nchini humo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2023.

Saa chache kabla ya hapo, Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Niger ilitangaza kupiga marufuku ndege zote za Ufaransa kupitia kwenye anga ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya Wakala wa Usalama wa Usafiri wa Anga wa Afrika, baraza la kijeshi la Niger limeamua kupiga marufuku ndege zote za Ufaransa kupita kwenye anga ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.