Sep 30, 2023 15:44 UTC
  • Sudan Kusini: Benki ya BRICS ni mwanzo wa mwisho wa udhibiti wa sarafu ya dola

Waziri wa Mambo ya Rais wa Sudan Kusini amesema kuwa, kudhihiri kwa Benki mpya ya NDB ya kundi la madola yanayoinukia kiuchumu la BRICS utakuwa mwanzo wa kusambaratika udhibiti wa sarafu ya dola ya Marekani katika miamala ya kifedha duniani kote.

Barnaba Benjamin amesema kwamba utawala wa Benki ya Dunia utaisha hivi karibuni kwa kupanuliwa zaidi matawi ya benki za maendeleo za kundi la BRICS la mataifa yanayoibukia kiuchumi.

Waziri huyo wa Sudan Kusini amesisitiza kuwa, masharti ya benki mpya za maendeleo za kundi la BRICS yanavutia sana, kwa sababu, tofauti na Benki ya Dunia, unaweza kunufaika haraka na suhula za kifedha za benkki hizo.

Afisa huyu ameongeza kuwa, sambamba na upanuzi wa benki za maendeleo ambazo ni wanachama wa kundi la BRICS, hivi karibuni tutashuhudia mwisho wa utawala na udhibiti wa kimataifa wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia.

Wakati huo huo, Waziri wa Fedha wa Russia amedokeza kuwa, nchi wanachama wa kundi la BRICS zinajiandaa kuanzisha mfumo wa mawasiliano ya kibenki kama mbadala wa ule wa SWIFT wa Wamagharibi.

Anton Siluanov amenukuliwa akisema hayo na shirika la habari la TASS na kueleza kuwa, suala hilo la kuanzisha mfumo mbadala wa SWIFT litajadiliwa na nchi wanachama wa BIRCS katika mkutano wa jumuiya hiyo ya kiuchumi mwaka ujao.

Japokuwa mtandao wa SWIFT unadai kwamba, haupendelei upande wowote katika masuala ya kisiasa lakini imebainika wazi kuwa, Marekani na nchi nyingine za Magharibi zinautumia mfumo huo kama wenzo wa kufanikisha malengo ya siasa zao za nje na za kifedha.

Katika kujibu vikwazo vya Magharibi dhidi ya Russia kwa kisingizio cha vita vya Ukraine, Moscow inafanya juhudi za kufanya biashara kwa kutumia sarafu za kitaifa. 

Kwa kuzingatia changamoto za hivi karibuni za kifedha duniani na sera kali za kigeni za Marekani, nchi wanachama wa BRICS zinataka kuchukua hatua za kupunguza utegemezi wa kimataifa kwa dola ya Marekani na sarafu ya nchi za Ulaya, euro.

Kundi la BRICS linaundwa na nchi za Russia, Brazil, India, China na Afrika Kusini. 

Nchi za Argentina, Misri, Ethiopia, Jamhuri ya Kiislamuu ya Iran, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu pia zimealikwa kuujiunga na kundi hilo.

Tags