Dec 02, 2023 10:33 UTC
  • Idadi ya waliofariki kutokana na mripuko wa kipindupindu nchini Ethiopia yafikia watu 400

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limetangaza kuwa, mripuko wa kipindupindu unaoendelea nchini Ethiopia, hadi hivi sasa umeshasababisha vifo vya zaidi ya watu 400 kufikia sasa.

Taarifa ya hivi karibuni kabisa ya masuala ya afya ya Ethiopia imeonya kwamba mafuriko yanayoendelea katika maeneo tofauti ya nchi hiyo yamezidisha maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu nchini humo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kuna ongezeko la asilimia 12 la vifo vinavyotokana na ugonjwa wa kipindupindu katika mwezi ulioisha wa Novemba ikilinganishwa na mwezi uliopita wa Oktoba, huku kesi 28,333 za kipindupindu zikiripotiwa kufikia Novemba 29, vikiwemo vifo vya wagonjwa 404.

Taarifa hiyo ya WHO aidha imesema: Huku kukiwa na ongezeko la idadi ya vifo vinavyotokana na kipindupindu, pia kuna ongezeko wagonjwa, na kufikia asilimia 1.43 mwishoni mwa Novemba, ikilinganishwa na asilimia 1.37 mwanzoni mwa mwezi huo wa Novemba.

Ripoti hiyo pia imeonesha kuongezeka idadi ya wilaya zilizokumbwa na milrpuko ya kipindupindu kutoka 81 iliyoripotiwa Novemba 1 hadi 97 ilipofika Novemba 29.

Watoto wa Ethiopia

 

Shirika hilo limeongeza kuwa, mripuko wa kipindupindu umedhibitiwa katika wilaya 198 kati ya wilaya 295 zilizoripoti wagonjwa wa kipindupindu tangu lilipoanza wimbi jipya la ugonjwa huo mwezi Agosti 2022.

Mwishoni mwa mwezi ulioisha wa Novemba, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilitoa indhari baada ya makumi ya watu kuaga dunia huku mamia ya wengine wakiathiriwa kutokana na mripuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika maeneo ya kusini mashariki mwa Ethiopia. 

Wakati huo taarifa ya OCHA ilisema kuwa, mripuko huo mpya wa kipindupindu umeenea katika maeneo 41 ya wilaya nne za jimbo la Oromia, na wilaya mbili za jimbo la Somali huko Ethiopia.

Tags