Dec 06, 2023 12:11 UTC
  • Mali na Niger zafuta mapatano kikoloni ya kodi na Ufaransa

Serikali za Mali na Niger zimetangaza kubatilisha mikataba miwili na Ufaransa ya ushirikiano na usaidizi wa kiutawala katika masuala ya kodi.

Nchi hizo mbili za Afrika Magharibi zinaongozwa na wanajeshi waliochukua madaraka katika mapinduzi yaliyoungwa mkono na wananchi waliochoshwa na sera za kikoloni za Ufaransa katika nchi hizo.

Katika kufuata matakwa ya wananchi, serikali za Mali na Niger zimekuwa zikichukua hatua za kujitenga na Ufaransa, mtawala wao wa zamani wa kikoloni.

Taarifa hiyo ya pamoja ya nchi hizo mbili imesema: "Mtazamo wa uhasama unaoendelea wa Ufaransa dhidi ya mataifa yetu... ulishadidisha ukosefu wa mlingano katika mikataba hii na kusababisha hasara kubwa kwa Mali na Niger. Ufaransa haijatoa jibu kwa  taarifa hiyo ya pamoja, ambayo imewekwa katika tovuti ya wizara ya mambo ya nje ya Mali.

Idadi kubwa ya nchi za magharibi na kati mwa Afrika bado hazina sarafu ya kitaifa kwani zingali zinategemea sarafu ya Ufaransa inayojulikana kama Faranga. Utegemezi huu unamaanisha kuwa nchi hizo zinashurutishwa kuweka fedha zao katika Benki Kuu ya Ufaransa ambayo hutoa idhini ya kutumiwa fedha hizo inavyotaka.

Hatua hiyo ya Mali na Niger ya kujitenga na mfumo wa kodi wa Ufaransa ni mwendelezo wa harakati za kujikomboa kutoka kwenye ukoloni mamboleo wa nchi za Magharibi kama Ufaransa. Watu wa nchi za ukanda wa Sahel Afrika wanataka demokrasia ya kweli, kuboreshwa uchumi na hali zao za kimaisha na kiusalama, na ndiyo maana wameunga mkono mapinduzi ya kijeshi yanayoziondoa madarakani serikali na tawala tegemezi kwa nchi za kikoloni.