Dec 08, 2023 03:17 UTC
  • Mahakama ya Afrika Magharibi yatupilia mbali pingamizi la vikwazo kwa uongozi wa kijeshi wa Niger

Mahakama ya Afrika Magharibi Jana imetupilia mbali kesi iliyowasilishwa na uongozi wa kijeshi wa Niger kwa ajili ya kuiondolea nchi hiyo vikwazo ilivyowekewa na jumuiya ya kikanda ya Ecowas baada ya mapinduzi nchini humo.

Wanajeshi wa kikosi cha Gadi ya Rais wa Niger Julai 26 mwaka huu walimtia nguvuni Rais Mohamed Bazoum na kisha kuunda kile walichokitaja kama "serikali ya mpito". 

Serikali hiyo ya mpito ya Niger imeiambia Mahakama ya Haki ya Jumuiya ya Ecowas yenye makao yake katika mji wa Abuja nchini Nigeria kwamba vikwazo dhidi ya Niger vilivyojumuisha nchi jirani kufungia Niger mipaka yao na Nigeria na kukata huduma ya umeme kwa nchi hiyo vimesababisha uhaba wa dawa za matibabu na chakula na hivyo kusababisha matatizo kwa wananchi. 

Hata hivyo Mahakama ya Haki ya Jumuiya ya Ecowas imetupilia mbali kesi hiyo iliyofunguliwa na serikali ya mpito ya Niger ikisema kuwa uongozi wa sasa wa kijeshi wa nchi hiyo haukuwa na sifa za kufungua kesi kwa niaba ya Niger. Jaji Dupe Atoki amesema kuwa ungozi wa kijeshi wa Niger si serikali inayotambulika na si mwanachama wa jumuiya ya Ecowas; kwa hiyo haustahiki kufungua kesi kama hii." 

Jaji, Dupe Atoki 

Hii ni katika hali ambayo viongozi wa ECOWAS wanatazamiwa kukutana mjini Abuja nchini Nigeria Jumapili ijayo kwa mkutano wa kilele wa kila mwaka ambao utajadili hali ya Niger.

Tags