Dec 08, 2023 03:18 UTC
  • Hali ya hatari yatangazwa Ushelisheli baada ya mlipuko na mafuriko makubwa

Visiwa vya Ushelisheli vimetangaza hali ya hatari na kuwataka wakazi wake kusalia majumbani baada ya mlipuko uliotokea katika ghala la vilipuzi na mafuriko.

 Taarifa ya Ofisi ya Rais wa Ushelisheli kwa vyombo vya habari imesema kuwa, Rais wa nchi hiyo ametangaza hali ya hatari "kufuatia mlipuko uliotokea kwenye ghala la CCCL la vilipuzi na kusababisha uharibifu mkubwa, na madhara makubwa yaliosababishwa na mvua."

Taarifa hiyo imesema: "Shule zote zitafungwa na wafanyakazi walioajiriwa katika sekta muhimu pekee ndio watakaoruhusiwa kusafiri, ili kuruhusu huduma za dharura kufanya kazi yao muhimu." 

Mlipuko huo ulitokea katika eneo la viwanda la Providence huko Mahé na kusababisha uharibifu mkubwa na katika eneo jirani. Mahé ndicho kisiwa kikubwa zaidi kati ya visiwa vya Ushelisheli, ambapo 87% ya wakazi 98,000 wanaishi katika kisiwa hicho.

Ushelisheli

Nchi ya Ushelisheli iliyoko katika Bahari ya Hindi na ni koloni la zamani la Uingereza, inajulikana kwa fukwe zake za mchanga mweupe na utalii wa kifahari, na inaundwa na visiwa 115.

Kanda ya Afrika Mashariki na Bahari ya Hindi zimeathiriwa na mvua kubwa na mafuriko yanayohusishwa na mabadiliko ya tabianchi ya El Niño kwa wiki kadhaa, ambayo yamewalazimisha zaidi ya watu milioni moja kuyahama makazi yao nchini Somalia na kusababisha vifo vya zaidi ya 300 katika ukanda huo.