Feb 26, 2024 07:25 UTC
  • Algeria yafungua msikiti mkubwa zaidi barani Afrika

Msikiti mkubwa zaidi barani Afrika, unaobeba waumini 120,000, ulifunguliwa nchini Algeria siku ya Jumapili.

Msikiti huo umezinduliwa baada ya miaka mingi ya ujenzi kusimama kutokana na gharama kubwa.

Msikiti huo ambao unajulikana kama Djamaa El-Djazair, umejengwa kwa usanifu majengo wa kisasa katika eneo lenye ukubwa wa hekta 27.75 (karibu ekari 70), na unatajwa kuwa wa tatu kwa ukubwa duniani baada ya misikiti miwili huko Makka na Madina, maeneo matakatifu zaidi ya Uislamu, huko Saudi Arabia. Ukumbi wake wa swala unaweza kuchukua watu 120,000.

Msikiti Mkuu wa Algiers uliojengwa na kampuni ya ujenzi ya China katika miaka ya muongo wote wa 2010, pia una mnara mrefu zaidi duniani, wenye urefu wa mita 265. Muundo wake wa kisasa umeiga mitindo ya ujenzi ya Kiarabu na Afrika Kaskazini na unaenzi mila na tamaduni za Algeria. Msikiti huo una maktaba ambayo inaweza kuhifadhi hadi vitabu milioni 1.

Rais wa Algeria Abdelmajid Tebboune aliuzindua msikiti huo, akitimiza ahadi yake ya kuufungua kwa fahari na hali nzuri.

Msikiti huo umefunguliwa rasmi kwa umma kwa wakati kutokana na kukaribia  mwezi mtukufu wa Ramadhani, ambapo Waislamu hukithirisha ibada.

Abdelaziz Bouteflika

Mbali na ukubwa wake, msikiti huo pia unajulikana kwa ucheleweshaji na mabishano yaliyohusisha miaka saba ambayo ulikuwa chini ya ujenzi, ikiwa ni pamoja na eneo la ujenzi, ambalo wataalam walionya lina hatari ya kukumbwa na tetemeko. Serikali ilikanusha taarifa kuwa eneo hilo lina hatari ya kukumbwa na tetemeko haribifu la ardhi.

Gharama rasmi ya mradi huo imetajwa kuwa dola milioni 898.

Msikiti huo awali ulikuwa mradi wa rais wa zamani hayati Abdelaziz Bouteflika, ambaye alianza ujenzi wake akiwa na nia ya kuufanya uwe mkubwa zaidi barani Afrika.

Alitaka uwe urithi wake na akauita "Msikiti wa Abdelaziz Bouteflika" kama ulivyo Msikiti wa Hassan II huko Casablanca, Morocco. Msikiti huo, uliopewa jina la Mfalme wa zamani wa Morocco - jirani ya Algeria na hasimu wake wa kikanda - uliwahi kutajwa kama msikiti mkubwa zaidi barani Afrika.

Lakini maandamano yaliyoikumba Algeria mwaka 2019 na kumfanya ajiuzulu baada ya miaka 20 madarakani yalizuia Bouteflika kutekeleza azma yake ya kuupa msikiti huo jina lake au kuuzindua Februari 2019 kama ilivyopangwa.