Mar 03, 2024 12:18 UTC
  • Ripoti: Jeshi la Burkina Faso latangaza kumuua kinara wa kundi la kigaidi

Jeshi la Burkina Faso limetangaza kumuua kinara wa kundi la kigaidi linalofungamana na mtandao wa Al-Qaeda ajulikanaye kama Hassan Idrissa Boli

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Burkina Faso, AIB, wanajeshi pia waliwaangamiza magaidi wapatao 26 wa kundi hilo ambalo kwa kifupi linajulikana kama JNIM kufuatia mapigano makali kwenye mpaka wa majimbo ya Mouhoun na Nayala nchini humo.
Tangu 2019, Boli aliripotiwa kuwa kinara wa magaidi katika majimbo ya Kossi na Banwa magharibi mwa Burkina Faso, na pia kuunda moja ya kambi kubwa zaidi za kigaidi katika mkoa huo katika kijiji cha Kinsere nchini humo.

Kwa mujibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali, raia na wanajeshi wasiopungua 10,000 wameuawa na magaidi, wanaoendesha shughuli zao nchini humo tangu 2015. Takriban wakazi milioni 2 wa Burkina Faso wamelazimika kuyahama makazi yao.

Takriban nusu ya Burkina Faso iko nje ya udhibiti wa serikali, kwani makundi yenye silaha yameharibu nchi hiyo kwa miaka mingi. Waasi na magaidi wameua maelfu ya watu na kupelekea  watu zaidi ya milioni mbili kuwa wakimbizi, jambo linalotishia uthabiti wa taifa hilo ambalo lilikumbwa na mapinduzi mawili ya kijeshi mwaka 2022.

Rais Traore wa Burkina Faso

Kwa muongo mmoja sasa, Burkina Faso imekuwa ikikabiliana na machafuko yanayohusishwa na makundi ya kigaidi ya al-Qaeda na Daesh/ISIS.

Wanajeshi wa Ufaransa walikuwa nchini Burkina Faso kwa zaidi ya miaka kumi kwa kisingizio cha kuisaidia nchi hiyo kupambana na ugaidi. Hata hivyo, magaidi walipata nguvu zaidi wakati wa uwepo wa wanajeshi wa Ufaransa nchini humo.

Kutokana na hali hiyo, mwaka jana serikali ya kijeshi iliamuru wanajeshi wa Ufaransa kuondoka nchini mara moja. Russia sasa inaisaidia Burkina Faso katika mapambano yake dhidi ya ugaidi na kuna matumaini kuwa mashambulizi ya kigaidi yatapungua kwa kiasi kikubwa katika miezi ijayo.