Apr 12, 2024 07:40 UTC
  • Wataalamu wa kijeshi wa Russia wawasili Niger kutoa msaada katika vita dhidi ya ugaidi

Wataalamu wa kijeshi kutoka Russia wamewasili nchini Niger kutoa mafunzo kwa vikosi vya ndani ya kupambana na ugaidi wiki chache baada ya nchi hiyo kutangaza kufuta mapatano yake ya kijeshi na Marekani.

Shirika la utangazaji la serikali ya Niger RTN Alhamisi limeonyesha ndege ya kijeshi ya Russia aina ya Iliyishin-76 ikitua huko Niamey. Mtangazaji aliripoti kwamba ndege hiyo ya kijeshi imewasili nchini umo baada ya mazungumzo ya hivi majuzi kati ya Rais wa Russia Vladimir Putin na Abdourahmane Tchiani, rais wa nchi hiyo ambaye rasmi anajulikana kama mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Niger la Ulinzi wa Nchi.

Wakijadili ajenda ya uhusiano wa nchi mbili, Putin na Tchiani walieleza nia ya kuimarisha mazungumzo ya kisiasa na kuendeleza ushirikiano wa kunufaishana katika maeneo mbalimbali.

Televisheni ya Niger imesema wataalamu hao wa Russia mbali na kutoa mafunzo ya vita dhidi ya ugaidi pia wataweka mfumo wa ulinzi wa anga, na kuongeza kuwa wakufunzi wa Russia watatoa mafunzo bora kwa wanajeshi wa Niger juu ya uendeshaji wa mfumo huo. Hivi karibuni Niger ilitangaza kubatilisha mapatnao yake ya kijeshi na Marekani miezi michache baada ya kufuta mapatano yake ya kijeshi na Ufaransa na kumtimua balozi wa Ufaransa nchini humo. Niger imelaumu madola hayo ya Magharibi kwa kuendeleza sera za kibeberu na kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo.