Apr 13, 2024 11:51 UTC
  • Infotrak yafichua: Nusu ya Wakenya waamini nchi inaelekea pabaya

Utafiti uliofanywa na kampuni ya Infotrak umeonyesha kuwa zaidi ya nusu ya Wakenya wanaamini nchi inaelekea vibaya.

Ni asilimia 19 pekee ya Wakenya wanaoamini kuwa, nchi inaendeshwa vyema huku wengi wakitaja gharama ya maisha kama sababu ya nchi kuelekea vibaya.

“Idadi ya Wakenya ambao wametaja gharama ya juu ya maisha kama suala kuu linaloibua wasiwasi imeongezeka kutoka asilimia 56 mnamo Desemba 2023 hadi asilimia 58 Machi 2024,” ulmesema utafiti huo.

Iliyokuwa mikoa ya Pwani, Nyanza na Magharibi ndio yenye idadi kubwa zaidi ya Wakenya wanaoamini nchi inaelekea pabaya kwa asilimia 70, 68 na 64 mtawalia.

Kwa upande mwingine, Wakenya wanaoishi katika maeneo ya Bonde la Ufa na Nairobi wanachangia asilimia kubwa zaidi ya wale wanaoamini kuwa nchi inaendeshwa vyema kwa asilimia 32 na 21 mtawalia.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti ya utafiti huo, meneja mkuu wa shughuli za nyanjani wa Infotrak, Johvine Wanyingo, amesema gharama ya juu ya maisha na utozwaji ushuru mkubwa ni masuala makuu yanayowatia Wakenya wasiwasi.

Wanaoamini kuwa nchi inaelekea pazuri wametaja sababu kuu kuwa ni kuwepo kwa amani nchini.

Johvine Wanyingo aneena: “Kumekuwa na amani nchini kwa muda. Kura ya maoni hata hivyo ilifanywa wakati mgomo wa daktari ulikuwa haujaanza na matokeo yangekuwa tofauti sana.”

Wakenya walitaja Seneti na Mahakama kama taasisi wanazoamini zinafanya vyema nchini kwa kupata alama B ya asilimia 69 na 67 mtawalia.