May 29, 2024 09:16 UTC
  • Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yatangaza serikali mpya baada ya kuchelewa kwa miezi kadhaa

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza serikali mpya leo Jumatano, na hivyo kuhitimisha sintofahamu ya kisiasa ya zaidi ya miezi mitano tangu kuchaguliwa tena rais wa nchi hiyo Felix Tshisekedi.

Baraza jipya la Mawaziri la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo lina mawaziri 54 akiwemo Waziri Mkuu Judith Suminwa Tuluka. Bi Tuluka ni Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke kuteuliwa huko Kongo mapema mwezi Aprili mwaka huu.

Waziri Mkuu, Judith Suminwa Tuluka

Rais Felix Tshisekedi amemteua Jacquemain Shabani kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Shabani ni Mkurugenzi wa  zamani wa kampeni za uchaguzi wa Tshisekedi ambaye pia alikuwa mshauri wake mkuu wa masuala ya kisiasa na uchaguzi. 

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amemteuwa pia mwanamana Therese Kayiwamba kuwa Waziri wa Mambo ya Nje akichukua nafasi ya Christophe Lutundula. 

Baraza jipya la mawaziri la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo lenye mawaziri wanawake 16 limeundwa baada ya miezi sita ya mashauriano kati ya washirika wapya wa Rais ambao wanadhibiti bunge la taifa kwa asilimia 95 ya viti vya wabunge tangu kufanyika uchaguzi wa mwisho Disemba mwaka jana. 

Haya yote yanajiri ambapo jeshi la Kongo wiki iliyopita lilitangaza kuwa limezima jaribio la mapinduzi katika mji mkuu wa nchi hiyo Kinshasa na kuwatia mbaroni watu kadhaa kwa kuhusika katika njama hiyo. 

Tags