May 29, 2024 10:11 UTC
  • Wananchi wa Afrika Kusini wapiga kura katika uchaguzi mkuu; Ramaphosa asema ANC itaibuka na ushindi

Wananchi wa Afrika Kusini leo Jumatano wamepiga kura katika uchaguzi mkuu ambao umetajwa kuwa ni muhimu sana kwa nchi hiyo katika kipindi chote cha miaka 30 iliyopita.

Chama cha African National Congress kimekuwa madarakani huko Afrika Kusini kwa miongo mitatu sasa. Chama hicho kilifanikiwa  kuuangusha utawala wa kikatili wa wazungu walio wachache  mwaka wa 1994. Sasa kumejitokeza vuguvugu la kizazi kipya ambacho hakiridhishwi na hali ya maisha ya wananchi wa Afrika Kusini. Nusu ya jamii ya watu milioni 62 wa Afrika Kusini wanakadiriwa kuishi katika lindi la umaskini. 

Baada ya kupiga kura yake, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema kuwa hana shaka yoyote kwamba chama chake cha ANC kitashinda kwa kura nyingi na kuendelea kuliongoza taifa hilo. 

Rais Cyril Ramaphosa baada ya kupiga kura katika mji wa Soweto 

Afrika Kusini pamoja na kuwa na uchumi ulionawiri barani Afrika lakini ina matatizo makubwa ya kiuchumi na kijamii ikiwemo asilimia 32 ya ukosefu wa ajira. Umaskini na ukosefu wa ajira unaowatesa raia wengi weusi wa Afrika Kusini vinatishia kukiondoa mdarakani chama tawala cha ANC ambacho kimeahidi kutatua matatizo hayo chini ya kauli mbiu yake ya "maisha bora kwa wote." 

Samuel Ratshalingwa, mmoja wa wananchi wa Afrika Kusini aliyekuweko katika safu ya kupiga kura katika shule moja huko Soweto ambako Rais Ramaphosa pia alipiga kura amesema kuwa kilio kikuu cha wananchi wa Afrika Kusini ni ukosefu wa ajira. Kura za maoni zinasema kuwa chama tawala cha ANC mara hii huwenda kikapoteza udhibiti wake bungeni baada ya kushinda chaguzi kuu sita mfululizo nchini humo.