May 30, 2024 09:26 UTC
  • Zoezi la kuhesabu kura Afrika Kusini laendelea huku ANC ikikabiliwa na uwezekano wa kupoteza viti

Zoezi la kuhesabu kura linaendelea Afrika Kusini baada ya uchaguzi wa Jumatano uliokuwa na ushindani mkali huku chama tawala ANC kikikabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa wanasiasa waliojiondoa katika chama hicho. Matokeo ya awali yanaonyesha ANC itapoteza wingi wa viti bungeni.

Tume Huru ya Uchaguzi (IEC) imesema upigaji kura wa dakika za mwisho katika miji mikubwa ulipelekea kuongezwa muda wa kupiga kura.

Chama cha ANC kimetawala siasa za Afrika Kusini tangu 1994 wakati kiongozi wa ukombozi Shujaa Nelson Mandela aliposhinda uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia nchini humo.

Kura za maoni zinaonyesha kuwa ANC inaweza kushinda takribani asilimia 40 ya kura, kutoka asilimia 57 mwaka 2019, lakini hakuna chama cha upinzani kinachotarajiwa kupata zaidi ya asilimia 25 ya viti.

Iwapo ANC itafanya vyema na kupata karibu asilimia 50 inaweza kushirikiana na baadhi ya vyama ndogo na vyama vya kikanda vinavyoshiriki uchaguzi.

Iwapo itashuka hadi asilimia 40 italazimika kuunda muungano  na chama kimoja au vyote viwili vya siasa kali za mrengo wa kushoto vikiongozwa na viongozi wa zamani wa ANC. Vyama hivyo ni chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) cha Julius Malema au Mkhonto weSizwe (MK) cha rais wa zamani Jacob Zuma.