Jun 18, 2024 09:22 UTC
  • ANC: Vyama 5 vya siasa kushiriki katika serikali ya umoja wa kitaifa ya Afrika Kusini

Chama cha African National Congress (ANC) kimesema kuwa, vyama vitano vya kisiasa vimetia saini rasmi taarifa ya kushiriki katika serikali ya umoja wa kitaifa (GNU).

Katika taarifa yake, chama cha ANC kimevitaja vyama hivyo vitano kuwa ni chenyewe cha ANC pamoja na vyama vya Democratic Alliance, Inkatha Freedom Party, GOOD na Muungano wa Patriotic. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, muungano huo wa vyama vitano una viti 273 Bungeni yaani asilimia 68 ya viti katika Bunge la Afrika Kusini.

Sehemu moja ya taarifa hiyo ya ANC imesema: "Vipaumbele vya GNU na mpango wa kima cha chini zaidi vinaendana kikamilifu na ahadi na sera za muda mrefu za ANC. Tumejitolea kupigania ustawi wa kiuchumi kupitia mfumo shirikishi na endelevu, kuandaa nafasi za ajira, kuleta mageuzi ya ardhi, ujenzi wa viwanda na maendeleo ya miundombinu. Lengo letu ni kuunda jamii yenye haki sawa ambayo itapambana na umaskini, ukosefu wa uadilifu, usalama wa chakula, gharama kubwa ya maisha sambamba na kulinda haki za wafanyakazi na kutoa huduma bora za kimsingi."

Cyril Ramaphosa, kiongozi wa ANC, alichaguliwa tena na Bunge siku ya Ijumaa kuwa Rais wa Afrika Kusini kwa miaka mitano mingine.

Hayo yamekuja baada ya Jacob Zuma, Rais wa zamani wa Afrika Kusini kusema kuwa, chama chake kitaungana na muungano wa upinzani kuipinga serikali na pia ameshikilia msimamo wake wa kupinga matokeo ya uchaguzi wa bunge, mahakamani. Chama chake cha uMkhonto weSizwe (MK) kitaungana na kile cha Economic Freedom Fighters (EFF) cha Julius Malema kilichoshinda viti 39 bungeni katika bunge jipya la Afrika Kusini.