Jun 22, 2024 11:18 UTC
  • Rais wa Tunisia amfuta kazi waziri kwa vifo vya makumi ya Mahujaji Makka

Rais Kais Saied wa Tunisia amempiga kalamu nyekundu Waziri wa Masuala ya Dini wa nchi hiyo, Brahim Chaibi, akimbebesha dhima ya vifo vya makumi wa raia wa nchi hiyo, waliokuwa miongoni mwa malaki ya Mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Allah mjini Makka, Saudi Arabia mwaka huu.

Rais Kais Saied ameripotiwa kuchukua hatua hiyo ya kumfukuza kazi Waziri wa Masuala ya Dini wa nchi hiyo, kufuatia malalamiko na ukosoaji mkubwa kutoka kwa Watunisia ndani na nje ya nchi. 

Kwa akali raia 49 wa Tunisia walifariki dunia kutokana na joto kali wakati wa ibada ya Hija nchini Saudi Arabia, huku kiwango cha joto kikiripotiwa kupindukia nyuzi joto 50. Aidha makumi ya Watunisia walioenda Saudia kuhiji hawajakulikani walipo mpaka sasa.

Mamia ya Mahujaji wameripotiwa kufariki dunia wakati wa ibada ya Hija mwaka huu nchini Saudi Arabia kutokana na joto kali nchini humo. Aidha wengine wameaga dunia kutokana na mkanyagano wakati amali za nguzo hiyo ya tano ya Uislamu.

Akthari ya Mahujaji karibu 1,000 walioripotiwa kufariki dunia wakati wa ibada ya Hija wiki iliyopita huko Makka, mji mtakatifu zaidi wa Kiislamu magharibi mwa Saudi Arabia, ni raia wa Misri. 

Vifo vya Mahujaji mjini Makka

Vyanzo vya matibabu na usalama vya Misri vimeiambia Reuters kwamba, takriban Wamisri 530 walikufa walipokuwa wakishiriki ibada hiyo, kutoka idadi ya 307 iliyoripotiwa hapo awali.

Takriban Waislamu milioni mbili walielekea Saudi Arabia kutekeleza ibada ya Hija ya mwaka huu. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hija ya Saudi Arabia, Mahujaji zaidi ya milioni 1.8 kutoka nchi mbalimbali duniani, na takriban raia 222,000 wa Saudia na wakazi wa nchi hiyo wameshiriki Hija ya mwaka huu.

 

Tags