Jun 24, 2024 06:51 UTC
  • FAO yapata dola milioni 25 za kuboresha usalama wa chakula nchini Somalia

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limetangaza kuwa, limetia saini mradi wa dola milioni 25 kwa ajili ya kuboresha usalama wa chakula nchini Somalia.

Katika taarifa yake ya jana Jumapili, FAO imesema kuwa, mkataba huo unaoitwa TRANSFORM, ni sehemu muhimu ya mpango mpana wa Johwar Offstream Storage (JOSP) ambao unawashirikisha wadau mbalimbali.

Mradi huo unalenga kukarabati miundombinu muhimu na kukuza kilimo kinachozingatia hali ya hewa kwa wakulima wadogo wadogo katika mji wa Jowhar wa jimbo la Hirshabelle nchini Somalia.

Etienne Peterschmitt

 

Mwakilishi wa FAO nchini humo, Etienne Peterschmitt amepokea kwa furaha ufadhili huo mpya na kugusia umuhimu wake katika kuchangia kuimarisha usalama wa chakula na ustahimilivu kwa jamii zinazoishi kando ya Mto Shabelle. 

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo ya FAO imesema kuwa, mradi huo utawasaidia wakulima wa Somalia kuwapa usalama wakati wa mafuriko, kuwa na kilimo cha uhakika cha umwagiliaji maji na kuwasaidia kutumia ardhi yao kwa tija na  kwa muda mrefu.

Utiaji saini huo umekuja baada ya kuzinduliwa rasmi mpango wa JOSP huko Jowhar tarehe 6 mwezi huu wa Juni. Mpango huo unatarajiwa kuhakikisha kwamba karibu watu 370,000 wanapata maji ya uhakika katika wilaya tano, kupunguza hatari ya mafuriko kwa watu milioni 1.5 na kupunguza athari za ukame kwa watu milioni 1.65 nchini Somalia.