Ghazouani aongoza katika matokeo ya awali ya uchaguzi wa Rais Mauritania
(last modified Sun, 30 Jun 2024 06:56:57 GMT )
Jun 30, 2024 06:56 UTC
  • Ghazouani aongoza katika matokeo ya awali ya uchaguzi wa Rais Mauritania

Rais Mohamed Ould Cheikh Ghazouani wa Mauritania yupo kifua mbele huku ujumlishaji wa matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika jana Jumamosi ukiendelea.

Matokeo ya muda yaliyotangazwa jana usiku na Kamisheni ya Uchaguzi ya nchi hiyo yanaonesha kuwa, Ghazouani anaongoza kwa asailimia 49 ya kura, huku mshindani wake wa karibu, Biram Dah Abeid akipata asilimia 22 ya kura.

Ghazouani, 67, kamanda mwandamizi wa zamani wa jeshi la Mauritania, anatazamiwa kuibuka mshindi kwenye uchaguzi huo, ambapo anawania muhula wa pili. Alichaguliwa kwa awamu ya kwanza mwaka 2016 katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika yenye watu milioni 5. 

Februari mwaka huu, Rais huyo wa Mauritania alichukua rasmi wadhifa wa Mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Afrika (AU) katika Mkutano wa 37 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa umoja huo huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia.

Muda mfupi baada ya kupiga kura katika mji mkuu wa nchi hiyo Nouakchott jana Jumamosi, Rais Ghazouani alisema, "Kauli ya mwisho itatolewa na wapiga kura wa Mauritania. Naahidi kuheshimu uamuzi na chaguo lao."

Anachuana na wagombea sita katika uchaguzi wa mwaka huu, akiwemo mwanaharakati wa kupambana na utumwa, Biram Dah Abeid, ambaye aliibuka wa pili kwa kuzoa asilimia 18 ya kura katika uchaguzi wa mwaka 2019.