Gavana wa Khartoum: Maelfu ya wageni wanapigana katika safu za RSF dhidi ya serikali ya Sudan
(last modified Mon, 15 Jul 2024 07:00:16 GMT )
Jul 15, 2024 07:00 UTC
  • Ahmed Othman Hamza
    Ahmed Othman Hamza

Gavana wa Jimbo la Khartoum, Ahmed Othman Hamza, amefichua kwamba mamlaka ya serikali imewataka wageni wanaoishi nchini humo kinyume cha sheria kuondoka na kurejea katika nchi zao baada ya maelfu yao kuhusika katika mapigano ya ndani wakishirikiana na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) dhidi ya jeshi la taifa.

Ahmed Othman Hamza ameeleza kuwa baada ya kuanza vita, raia wa kigeni wamesambaa kwenye makazi ya watu mjini Khartoum, na baadhi yao wanashirikiaina na wapiganaji wa Vikosi vya Msaada wa Haraka na kuwa tishio kwa usalama na utulivu, akibainisha kuwa idadi yao inafikia makumi ya maelfu.

Gavana wa Jimbo la Khartoum amesema kuwa 60% ya wakazi wa jimbo hilo waliondoka baada ya kuanza vita, ama kwa hiari yao ili kuepuka hatari ya mapigano, au kwa kwa nguvu baada ya wanamgambo wa RSF kuwalazimisha kuondoka kwenye nyumba zao. Amesema waliokataa kuondoka wameuawa na kuzikwa kwenye nyumba zao, na wengine miili yao iliachwa wazi na kuliwa na mbwa.

Mapema mwezi huu wa Julai, Mkuu wa Baraza la Utawala wa Sudan, Abdel Fattah Al-Burhan, alisema kuwa wanamgambo wa kundi la Daesh wanapigana katika safu ya Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vinavyoongozwa na Muhammad Hamdan Dagalo (Hemedti), akisisitiza kuwa jeshi la Sudan linapinga makubaliano yoyote ambayo hayatanguliwi na kuondolewa kwa vikosi vya RSF katika maeneo yanayodhibitiwa na kundi hilo.

Al-Burhan ambaye alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari huko Port Sudan, alisema wapiganaji wa RSF walishambulia vituo walikokuwa wakishikiliwa wanachama wa Daesh (ISIS) na kuwakomboa na sasa wanapigana katika safu zake.

Al-Burhan amesema, hatari ya wanamgambo hao ni miongoni mwa changamoto hatari zinazolikabili eneo hilo iwapo Sudan itaanguka, jambo ambalo amesisitiza kuwa nchi nyingi za eneo hilo hazilitambui.