Rais Ruto wa Kenya awarejesha mawaziri 6 wa zamani kati ya wateule 11, wengine kufuatia
(last modified Fri, 19 Jul 2024 15:03:19 GMT )
Jul 19, 2024 15:03 UTC
  • Rais William Ruto wa Kenya
    Rais William Ruto wa Kenya

Rais William Ruto wa Kenya amerudisha mawaziri sita wa zamani kati ya 11 aliowateua kwenye Baraza lake jipya la Mawaziri.

Majina mawaziri 11 walioteuliwa na Rais Ruto yatawasilishwa Bungeni ili kupigwa msasa kabla ya kuajiriwa rasmi kupitia hafla itakayofanyika Ikulu ya Nairobi.

Rais Ruto amemteua tena Kithure Kindiki kuchukua wadhifa ule ule aliokuwa nao wa Usalama wa Ndani, Aden Barre Duale amerejea kwenye Wizara ya Ulinzi, Soipan Tuya pia amerejeshwa kwenye Wizara ya Mazingira huku Davis Chirchir aliyekuwa katika Wizara ya Kawi akipewa Wizara ya Barabara na Uusafirishaji. Alice Wahome aliyekuwa katika Wizara ya Ardhi ameteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi. Rebecca Miano aliyekuwa Wizara ya Uwekezaji na Biashara amepewa jukumu la kuwa Mwanasheria Mkuu.

Rais Wiliam Ruto wa Kenya Ruto amesema kwamba hii ni awamu ya kwanza ya uteuzi, akimaanisha kwamba uteuzi wa wengine 11 utafanywa baadaye.

Haijajulikana bayana iwapo sura kamili ya “serikali jumuishi” aliyosema kwa msisitizo, itadhihirika kwenye uteuzi ujao au la, haswa kutokana na tetesi kwamba upande wa upinzani, hususan mrengo unaoongozwa na Raila Odinga, utajiunga na serikali.

Rais William Ruto alivunja Baraza la Mawaziri wiki iliyopita kutokana na mashinikizo na maandamano ya vijana wa kizazi cha Gen-Z. 

Vijana wa Gen-Z walianza kufanya maandamano mwezi uliopita kupinga Muswada wa Fedha wa 2024 ambao ungechangia kuongezeka viwango vya ushuru; lakini sasa yamebadilika na kuwa maandamano ya kukosoa utawala wa Rais Ruto.

Wandamanaji Kenya

Mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu yanasema kuwa, kwa uchache watu 50 wameshauawa katika maandamano hayo huku vyombo vya usalama vikilaumiwa kwa kutumia mabavu na kufyatua risasi dhidi ya waandamanaji.

Kiongozi huyo wa Kenya ameutuhumu Wakfu wa Ford wa Marekani (Ford Foundation), kuwa ndio unaochochea vurugu zinazoshuhudiwa nchini humo.