Aug 04, 2024 07:21 UTC
  • Takriban watu 23 wameuawa katika shambulizi la RSF huko El Fasher nchini Sudan

Takriban watu 23 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulio la mizinga lililofanywa na wapiganaji wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) huko El Fasher, makao makuu ya Jimbo la Darfur Kaskazini.

Kundi moja lisilo la kiserikali huko El Fasher limeripoti habari hiyo katika ukurasa wake wa Facebook na kuongeza kuwa, taarifa zilizopo hadi sasa zinaonesha kwamba, takriban raia 23 wameuawa na wengine 60 kujeruhiwa kutokana na kushambuliwa kwa makombora na RSF.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, pamoja na kuendelea kulenga vituo vya afya katika jimbo hilo, RSF jana Jumamosi ilishambulia pia kituo cha afya cha Tambasi kilichoko kusini mwa El Fasher.

Mamlaka za serikali huko El Fasher hazikuweza kupatikana ili kutoa maoni yao. Vikosi vya RSF navyo hadi wakati tunaandaa taarifa hii vilikuwa bado havijasema chochote kuhusu tukio hilo.

Tangu Mei 10 mwaka huu hadi hivi sasa, mapigano makali yamekuwa yakiendelea huko El Fasher kati ya Wanajeshi wa Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).

Sudan imekumbwa na mgogoro mbaya kutokana na uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi ya SAF na RSF tangu Aprili 15, 2023, na kusababisha vifo vya watu 16,650.

Takriban watu milioni 10.7 ni wakimbizi wa ndani nchini Sudan, huku takriban wengine milioni 2.2 wakikimbilia nchi jirani. Hayo ni kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa zilizotolewa Jumatatu iliyopita.