Aug 08, 2024 02:32 UTC
  • Niger yavunja uhusiano wa kidiplomasia na Ukraine; uamuzi huo umeanza kutelezwa mara moja

Niger imetangaza kuvunja mara moja uhusiano wake na kidiplomasia na Ukraine. Hayo yametangazwa na Amadou Abdramane, msemaji wa serikali ya Niger kwa njia ya televisheni.

Amesema katika taarifa yake hiyo kwamba, hatua hiyo imechukuliwa kwa sababu ya uungaji mkono wa Ukraine kwa magenge ya kigaidi, na amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoa uamuzi dhidi ya uchokozi wa Kyiv wa kuhatarisha usalama wa Niger. 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kwa kuzingatia uzito wa hali hiyo na kutokana na kuhusika Ukraine katika uvamizi wa Mali, serikali ya Niger inaungana na serikali ya Mali na wananchi wake kuvunja mara moja uhusiano wake wa kidiplomasia na Ukraine, na inalitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lichukue uamuzi madhubuti dhidi ya uchokozi wa Ukraine.

Niger imevunja mara moja uhusiano wake na Ukraine kutoka na Kyiv kukiri kuunga mkono magenge ya kigaidi

 

Siku ya Jumapili, serikali ya Mali ilisema imevunja mara moja uhusiano wa kidiplomasia na Ukraine na kusisitiza kuwa, Ukraine imehusika moja kwa moja katika ugaidi uliohatarisha usalama wa Mali.

Uamuzi huo umechukuliwa kujibu matamshi ya kifidhuli ya Andriy Yusov, msemaji wa idara ya ujasusi ya jeshi la Ukraine, ambaye hivi karibuni alikiri kuhusika kwa nchi yake katika shambulio la magenge ya kigaidi yaliyosababisha vifo vya maafisa wa ulinzi na usalama wa Mali. 

Tarehe 30 mwezi uliopita wa Julai, wanajeshi wa Mali walitangaza kuuliwa wanajeshi wake wengi wakati wa mapigano makali ya Julai 26 kati yao na magenge ya kigaidi ambapo baadaye Ukraine ilikiri kuyasaidia magenge hayo. 

Burkina Faso, Mali na Niger zimeunda Shirikisho la Muungano wa Nchi za Sahel na zimeamua kuwa na misimamo ya pamoja.