Aug 12, 2024 10:51 UTC
  • DRC na Zambia zaanza mazungumzo kufuatia kufungwa mpaka wa pamoja wa nchi mbili

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC ambayo ni ya pili duniani kwa uzalishaji wa madini ya shaba imesema imeanza mazungumzo na Zambia, siku moja baada ya jirani yake huyo wa kusini mwa Afrika kufunga mpaka wao wa pamoja, na hivyo kuziba njia kuu ya kusafirishia madini hayo ya DRC kupitia nchi hiyo.

Waziri wa Biashara wa Zambia Chipoka Mulenga alitangaza kufungwa kwa muda mpaka huo siku ya Jumamosi baada ya serikali ya Kongo DR kutangaza marufuku ya uagizaji vinywaji baridi na pombe iliyosababisha maandamano ya wasafirishaji wa Kongo katika mji wa Kasumbalesa kwenye mpaka wa pamoja na Zambia.
 
Hata hivyo wizara ya biashara ya DRC ilitoa taarifa hapo jana Jumapili na kueleza kuwa mazungumzo kati ya serikali ya nchi hiyo na ya Zambia yalianza jana hiyohiyo kwa njia ya video ili kuwezesha kufunguliwa mipaka kwa haraka.
 
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, katika saa zinazofuatia, pande hizo mbili zitakutana Lubumbashi huko Haut-Katanga kutafuta suluhu ya kudumu kuhusu biashara.
Julien Paluku Kahongya

Waziri wa Biashara wa Kongo DR Julien Paluku Kahongya alisema katika taarifa aliyotoa mapema jana kwamba wizara yake haikupokea notisi rasmi ya mzozo wa kibiashara kutoka Zambia kabla ya kutangaza kufunga mpaka.

Katika taarifa hiyo, Kahongya alielezea kwa kina makubaliano ya biashara ya nchi hizo mbili na taratibu zake za utatuzi wa migogoro.

Mwaka uliopita wa 2023 Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilikuwa ya pili duniani kwa uzalishaji na ya tatu kwa usafirishaji wa madini ya shaba kwa kuzalisha karibu tani milioni 2.84 ya madini hayo.

Zambia ni njia kuu ya usafirishaji kwa nchi hiyo ya Afrika ya Kati. Shaba nyingi ya Kongo DR inayosafirishwa kwa ajili ya kuuzwa nje ya nchi hupitia mji wa Kasumbalesa na kuingia Zambia.../