Ethiopia yawasamehe wanajeshi 178 waliohukumiwa kifo kwa uhalifu wakati wa vita vya Tigray
Wizara ya Ulinzi ya Ethiopia imetangaza leo Jumanne kuwa imewasamehe wanajeshi 178 waliohukumiwa kifo kwa kuhusika katika uhalifu uliotendwa wakati wa vita vya Tigray.
Taarifa ya Wizara ya Ulinzi wa Ethiopia imesema kuwa: "Hatua hiyo imechukuliwa kama sehemu ya msamaha wa kuadhimisha Mwaka Mpya wa Ethiopia."
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo, watu hao walitiwa hatiani na mahakama za kijeshi kwa kuacha majukumu yao ya kikatiba na kutenda makosa makubwa dhidi ya jeshi na wananchi wa Ethiopoia. Wanajeshi hao ni wale ambao tayari walikuwa wanatumikia vifungo vyao jela.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Msamaha huo umeidhinishwa baada ya kutolewa maombi rasmi ya kuhurumiwa wafungwa hayo na kupasishwa na Bodi ya Msamaha."
Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu, mgogoro wa Tigray ulianza mwezi Novemba 2020 wakati vikosi vya Tigray People's Liberation Front (TPLF) vilipoanza kushambulia kambi za jeshi la serikali na kusababisha vita vilivyopelekea kuuawa mamia ya maelfu ya watu na kuwafanya wakimbizi mamilioni ya watu wengine waliolazimika kuyahama makazi yao kutokana na vita vikali vilivyotokea baina ya pande hizo mbili, kama lilivyoripoti shirika hilo.
Mgogoro huo ulipungua baada ya kutiwa saini mikataba ya amani mjini Pretoria Afrika Kuisni na Nairobi Kenya mwezi Novemba mwaka jana.